Kampuni ya Sandaland Fashion Wear Limited imesema inakusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kufuatia kauli yake kuhusu jezi mpya zinazotajwa kuwa za Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo leo Septemba 18, 2026 imesema kauli ya Makonda imeathiri jina, hadhi na biashara ya kampuni hiyo, ambayo inadai kuwa inahusika katika uzalishaji na usambazaji wa jezi hizo kwa mujibu wa mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Hatua hiyo imekuja baada ya Makonda, Septemba 16, 2026, kuchapisha ujumbe kupitia akaunti yake ya Instagram, akieleza kutoridhishwa na jezi hizo na pia kuhoji matumizi ya picha ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), katika kuziwasilisha kwa umma ambapo kauli hiyo imeibua mjadala kuhusu jezi hizo pamoja na utaratibu uliotumika katika kuzitangaza.
Katika tamko lake, Sandaland imesema kauli hiyo si kauli ya kawaida kwa kuwa, kwa mtazamo wa kampuni, imehusisha moja kwa moja jina na bidhaa zake na inaweza kusababisha madhara ya kibiashara.
Aidha Kampuni hiyo imesema imepokea kwa masikitiko kauli hiyo na kwamba haitakaa kimya, huku ikisisitiza kuwa jezi hizo zimezalishwa na kusambazwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kimkataba na zimewahi kutumika na Timu za Taifa za wanaume na wanawake. “Sandaland inakusudia kuchukua hatua za kisheria juu ya kauli hiyo”, ikieleza kuwa tayari imeona madhara ya kiuchumi na ya kihadhi.
Chanzo cha mgogoro huo ni kauli iliyotolewa na Waziri Makonda kupitia Instagram, ambapo alikosoa ubora wa jezi hizo na kusema ofisi yake haikuwa na taarifa kuhusu matumizi ya picha ya Naibu Waziri. Waziri huyo alinukuliwa akisema: “Hii sio jezi ya Taifa Stars. Taifa Stars kwa ubora wake hatuwezi kuwa na jezi za kiwango cha chini hivi. Acheni kutumia picha za Naibu wangu huku ofisi yangu haina taarifa. Tuheshimiane.”