Wilaya ya Bukombe mkoani Geita inatarajiwa kuandika historia Agosti 4, 2026, kwa kuwa mwenyeji wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mwananchi, ambapo Klabu ya Yanga SC itatangaza rasmi kikosi chake cha msimu wa 2026/2027 sambamba na uzinduzi wa Uwanja Mpya wa Bukombe uliopo Ushirombo.
Mbali na kutambulishwa kwa kikosi hicho, hafla hiyo itaambatana na uzinduzi rasmi wa uwanja huo wa kisasa uliojengwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya michezo ya ndani na kimataifa, ukiwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya mashabiki 5,000.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika uwanja huo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskasi Muragili, amesema maandalizi ya maadhimisho hayo yanaendelea vizuri na kwamba kwa mara ya kwanza katika historia, Wiki ya Mwananchi itafanyika nje ya maeneo yake ya kawaida na kuhamia Ushirombo.
Muragili amesema uwanja huo umejengwa kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya michezo katika Wilaya ya Bukombe na Mkoa wa Geita kwa ujumla, huku ukitarajiwa kuwa kitovu cha mashindano na matukio mbalimbali ya michezo.
Amewahimiza wananchi wa Bukombe, Mkoa wa Geita na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo muhimu litakalowakutanisha mashabiki wa soka, viongozi mbalimbali na wapenzi wa Klabu ya Yanga kutoka maeneo tofauti nchini.
baada ya shughuli ya utambulisho wa kikosi cha Yanga kukamilika, kutachezwa mchezo wa kirafiki kati ya Geita Gold FC, ambao ndio wenyeji wa uwanja huo, dhidi ya Pamba Jiji FC ya Mwanza ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa uwanja huo.
Kwa upande wao, baadhi ya wadau wa soka Wilayani Bukombe, akiwemo Katibu wa GEREFA Wilaya ya Bukombe, Bosco Mwidadi, wameeleza kuwa uzinduzi wa uwanja huo ni hatua kubwa ya maendeleo ya michezo wilayani humo, wakisema wanatarajia kuona mechi nyingi za ngazi ya juu zikichezwa katika uwanja huo baada ya kuzinduliwa rasmi.
Wamesema ujio wa maadhimisho ya Wiki ya Mwananchi Bukombe utatoa fursa ya kutangaza vivutio vya wilaya hiyo, kuhamasisha uchumi wa wananchi kupitia biashara mbalimbali pamoja na kuongeza hamasa ya maendeleo ya michezo katika Mkoa wa Geita.