Michuano ya soka ya Buhabi Cup inatarajiwa kuanza rasmi Julai 20, 2026 katika Kata ya Mgusu, Manispaa ya Geita, ikishirikisha timu nane kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana na kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa vya michezo kwa timu zinazoshiriki, Diwani wa Kata ya Mgusu ambaye pia ni mdhamini wa michuano hiyo, Yohana Buhabi, amesema mashindano hayo yameandaliwa ili kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji vya soka kuonyesha uwezo wao na kujitangaza mbele ya wadau mbalimbali wa mchezo huo.
Buhabi amesema michezo ni nyenzo muhimu ya kuwajengea vijana nidhamu, kuwawezesha kujiajiri kupitia vipaji vyao na kuimarisha mshikamano katika jamii. Aidha, amewataka washiriki kuzingatia sheria za mchezo, nidhamu na ushindani wa haki ili kufanikisha malengo ya mashindano hayo.

“Nia yetu ni kuona kila kijana mwenye kipaji anapata nafasi ya kukionyesha. Tunaamini kupitia Buhabi Cup kutapatikana vipaji vitakavyofika kwenye ngazi za juu za soka nchini,” amesema Buhabi.
Kwa upande wake, mratibu wa mashindano hayo, Faida Juma, amesema jumla ya timu nane zitashiriki katika michuano hiyo. Amesema mshindi wa kwanza atazawadiwa kombe pamoja na shilingi milioni moja, mshindi wa pili atapata shilingi 600,000, huku mshindi wa tatu akijinyakulia shilingi 300,000.
Naye Elizabeth Joseph kutoka Benki ya Azania amesema taasisi hiyo imeamua kudhamini michuano hiyo ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika maendeleo ya jamii, hususan kuwaunga mkono vijana kupitia michezo.
Michuano ya Buhabi Cup inatarajiwa kuwa chachu ya kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana katika Wilaya ya Geita, sambamba na kutoa burudani kwa wananchi na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wakazi wa Kata ya Mgusu na maeneo jirani.
