Latest Posts

MRADI WA YOUNG SINGLE MOTHERS WAREJESHA MATUMAINI KWA WASICHANA 197

 

Zaidi ya wasichana 197 waliopata ujauzito katika umri mdogo wamepata fursa ya kujenga upya maisha yao kupitia mradi wa Young Single Mothers unaotekelezwa na Shirika la Ilula Orphan Program (IOP), hatua inayolenga kurejesha matumaini na kuwawezesha kujitegemea baada ya kukumbana na changamoto mbalimbali.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Ilula Orphan Program (IOP), Edson Msigwa, amesema wasichana wengi waliopata ujauzito katika umri mdogo walijikuta wakitengwa na familia pamoja na jamii, hali iliyochangia kukatisha masomo yao na kuathiri ustawi wao wa kijamii na kiuchumi.

Msigwa amesema ukuaji wa mji wa Ilula umevutia watu kutoka maeneo mbalimbali, ambapo baadhi yao huwarubuni mabinti wadogo kwa ahadi mbalimbali, kuwapa ujauzito na baadaye kutoweka bila kutimiza wajibu wao, jambo linalowaacha wasichana hao wakikabiliwa na maisha magumu huku mzigo wa malezi ukibebwa na familia zao.

Ameeleza kuwa kupitia mradi wa Young Single Mothers, shirika hilo linawapatia wanufaika elimu ya kujitambua, afya ya uzazi na uzazi wa mpango, huduma za ushauri wa kisaikolojia pamoja na mafunzo ya ujasiriamali, ili kuwajengea uwezo wa kurejea katika maisha yenye tija na kujitegemea.

Aidha, ameongeza kuwa mradi huo unatoa fursa kwa wasichana hao kuendelea na elimu au kujifunza stadi mbalimbali za maisha kulingana na mazingira yao, hatua inayowasaidia kurejesha ndoto walizodhani zimefutika kutokana na ujauzito wa utotoni.

 

Baadhi ya wanufaika wa mradi huo wameeleza kwa hisia nzito namna walivyopitia changamoto za kupata ujauzito katika umri mdogo, zikiwemo unyanyapaa kutoka kwa jamii, kukataliwa na baadhi ya ndugu pamoja na kukosa matumaini ya maisha.

Hata hivyo, wamesema kupitia msaada wa Ilula Orphan Program (IOP), wamepata faraja, ushauri na uwezeshaji uliowarejeshea heshima, kujiamini na matumaini mapya ya kutimiza ndoto zao, huku wakitoa wito kwa wasichana wengine wanaokabiliwa na changamoto kama hizo kutokata tamaa bali kutafuta msaada utakaowawezesha kujenga upya maisha yao.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!