Latest Posts

“WAZAZI WASIWAFICHE WATOTO WENYE ULEMAVU, ELIMU NI HAKI YAO”-NGAJILO

 

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, amekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya elimu kwa watoto wenye maisha duni wanaosoma katika shule za msingi mkoani Iringa, huku akitoa wito kwa wazazi kuhakikisha watoto wote, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata haki yao ya elimu bila ubaguzi.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika Shule ya Msingi Ugele, Ngajilo alikabidhi magodoro, madaftari, mahindi, maharage, matranka na vifaa vingine muhimu vinavyolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na ustawi wa watoto hao.

Ngajilo aliwasihi wazazi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu majumbani, akieleza kuwa nao wana uwezo mkubwa wa kufanikiwa endapo watapata elimu na malezi bora akiibainisha kuwa wapo watu wengi wenye ulemavu waliopata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uongozi na uwakilishi wa wananchi.

Aidha, aliwapongeza walimu wanaowahudumia watoto hao kwa kujitolea licha ya changamoto zilizopo, akisema kazi yao ni wito unaohitaji moyo wa upendo, uvumilivu na uzalendo huku akiwataka wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu kwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kuwasaidia kufanya kazi za nyumbani ili kuongeza ufanisi wa masomo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, walimu, wazazi na wanafunzi. Ngajilo alieleza matumaini yake kuwa uwekezaji unaoendelea katika elimu utaiwezesha Iringa kuendelea kuzalisha wataalamu na viongozi mbalimbali watakaotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa, huku msaada huo ukitarajiwa kuboresha ustawi na fursa za elimu kwa watoto wenye maisha duni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!