Latest Posts

AIRTEL AFRICA YAAHIDI KUUNGANISHA SHULE 5,000 NA INTANETI YA BURE IFIKAPO 2027

Kampuni ya Airtel Afrika imetangaza mpango wa kuunganisha shule 5,000 na huduma ya intaneti ya bure ifikapo mwaka 2027 katika nchi 14 za Afrika inakotoa huduma, kupitia ushirikiano kati ya Airtel Afrika Foundation na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Akizungumza katika ziara yake kwenye Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Monika (St. Monica) mjini Lusaka, Zambia, Afisa Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema mpango huo unalenga kupanua upatikanaji wa elimu ya kidijitali kwa watoto wa Afrika kwa kushirikiana na serikali za nchi husika.

Alisema hadi sasa mradi huo wenye thamani ya dola milioni 57, ulioanzishwa mwaka 2021, umefanikiwa kuunganisha shule 3,296 na intaneti, huku zaidi ya wanafunzi milioni mbili pamoja na walimu karibu 40,000 wakinufaika. Aidha, maeneo 64 ya kujifunzia mtandaoni yameondolewa gharama za matumizi ya data (zero-rated), jambo lililoruhusu zaidi ya watu milioni 11 kupata maudhui ya elimu bila malipo.

“Wanafunzi wanapata elimu ya kiwango cha juu kupitia mtaala ulioandaliwa na UNICEF kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali za Elimu. Pia tunawajengea uwezo walimu kutumia teknolojia za kidijitali kufundisha kwa ufanisi. Tutaendelea kuimarisha upatikanaji wa intaneti ya bure mashuleni na majukwaa ya elimu yasiyotozwa gharama za data,” alisema Taldar.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Monika, Sr. Matilda Soloko, alisema shule hiyo ni miongoni mwa zilizonufaika katika awamu ya kwanza ya mradi huo nchini Zambia, na kwamba matumizi ya teknolojia yameongeza uelewa wa wanafunzi katika masomo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa UNICEF nchini Zambia, Dkt. Saja Farooq Abdullah, alisema ushirikiano huo unalenga kupunguza pengo la ujumuishi wa kidijitali na kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujifunza bila kujali mahali alipo.

Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari katika Wizara ya Elimu ya Zambia, Yvonne Mwemba Chuulu, alisema ushirikiano kati ya serikali, UNICEF na Airtel Africa umewezesha wanafunzi kujifunza kwa mfumo unaochanganya ufundishaji wa darasani na matumizi ya teknolojia, huku baadhi yao wakipata fursa ya kuendelea na masomo hata wakiwa nyumbani.

Mpango wa Kuunganisha Shule unatekelezwa katika nchi 13 ambazo ni Chad, Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Gabon, Kenya, Madagascar, Malawi, Niger, Nigeria, Rwanda, Tanzania, Uganda na Zambia. Kupitia mpango huo, shule hupatiwa huduma ya intaneti na walimu hupewa mafunzo ya matumizi ya zana za kidijitali ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, hususan katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.

Airtel Afrika Foundation inaeleza kuwa itaendelea kuwekeza katika elimu, ujumuishi wa kidijitali, ujumuishi wa kifedha na uhifadhi wa mazingira kama sehemu ya mkakati wake wa kuchochea maendeleo jumuishi barani Afrika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!