Ripoti zimeibua madai kuhusu uwepo wa mpango wa kijeshi unaofadhiliwa na Saudi Arabia nchini Somalia, unaolenga kuajiri wanajeshi kutoka maeneo mbalimbali na kuwapa mafunzo kupitia wakandarasi wa kijeshi wa kigeni (mercenaries), kabla ya baadhi yao kutumwa nchini Sudan kushiriki mapigano upande wa Jeshi la Sudan na washirika wake.
Kwa mujibu wa jukwaa la Sahih Al-Soudan, mafunzo hayo yanafanyika katika eneo la Guri Ceel, jimbo la Galmudug katikati mwa Somalia, ambapo vikosi vinavyotajwa kuwa vya “operesheni maalum” vinaandaliwa. Jukwaa hilo, likinukuu chanzo cha usalama nchini Somalia, linasema ujumbe wa kijeshi kutoka Saudi Arabia ulitembelea kambi mbili za mafunzo mnamo Juni 29, huku idadi ya askari wanaopatiwa mafunzo ikifikia takribani 5,107.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa karibu askari 2,000 kati ya wanaopatiwa mafunzo hayo wametoka Puntland, eneo la kaskazini mashariki mwa Somalia, na kwamba wanapitia mafunzo maalum yanayolenga kuwaandaa kwa operesheni za kipekee. Aidha, vyombo vya habari vya ndani vinadai kuwa Saudi Arabia imeajiri wakufunzi wa kijeshi kutoka Romania, Ukraine, Afrika Kusini na Colombia kusimamia mafunzo hayo kwa vikosi vinavyodaiwa kuwa vina utii kwa Rais Hassan Sheikh Mohamud.
Wakati huo huo, Sahih Al-Soudan inasema taarifa hizo zinaungwa mkono na ushuhuda wa baadhi ya wakazi wa Guri Ceel, ambao wamedai kushuhudia ongezeko la shughuli za kijeshi katika wiki za hivi karibuni, ikiwemo kuwasili kwa makundi ya waajiriwa wapya, misafara ya magari ya kijeshi na uwepo wa watu wa kigeni waliovalia sare za kijeshi.
Ripoti hiyo pia inaibua maswali kuhusu sababu za kupewa kipaumbele kwa waajiriwa kutoka Puntland. Mwandishi na mtafiti mmoja wa masuala ya Pembe ya Afrika, ambaye hakutaka kutajwa kwa sababu za kiusalama, alinukuliwa akisema uchaguzi huo huenda unahusiana na uwezo wa kiusalama wa Puntland, ambayo tangu mwaka 1998 imekuwa na utawala wa kujitegemea ndani ya mfumo wa shirikisho la Somalia.
Kwa mujibu wa mtafiti huyo, Puntland ina taasisi za usalama zilizoimarika zaidi kuliko maeneo mengine ya Somalia na ina uzoefu mkubwa wa kupambana na makundi yenye silaha, hususan Al-Shabaab na kundi la Islamic State katika milima ya Golis. Aliongeza kuwa eneo hilo lina wanajeshi wenye uzoefu wa mapigano na nidhamu ya kijeshi, jambo ambalo linaweza kuwa sababu ya kuchaguliwa kwa idadi kubwa ya waajiriwa kutoka Puntland kwa ajili ya kikosi hicho kinachodaiwa kuandaliwa kwa operesheni maalum.
Serikali ya Somalia na Saudi Arabia hazijatoa tamko rasmi kujibu madai hayo hadi wakati wa kuandaliwa kwa taarifa hii.