Theophilida Felician, Dodoma.
Wataalamu wa tiba asili washauriwa kupata elimu shirikishi yenye kuwasaidia na kuwaongoza kufanya kazi ya kutoa tiba ya asili kitaalamu zaidi.
Wito huo umetolewa na katibu mkuu wa chama cha waganga watiba asili nchini TAMESOT Bw Lukas Joseph Mlipu wakati akizungumza na chombo hiki akiwa makao makuu ya ofisi za chama hicho Kibaigwa Dodoma.

Katibu mkuu Mlipu amesema kuwa ipo haja ya kuwepo kwa maboresho makubwa katika taaluma ya tiba asili ili kuhakikisha tiba hiyo inabakia salama na kuendelea kutoa tiba bora kwa jamii.
Ameyataja miongoni mwa maboresho yanayopaswa kutiliwa mkazo ni pamoja na kupewa kipaumbele suala la elimu kwa wataalamu hao ili kuwasaidia kutoa huduma yenye kufuata kanuni, miongozo na sheria za tiba asili kama inavyoelekezwa na serikali kupitia baraza la tiba asili na tiba mbadala.
Amefafanua kuwa wao kama TAMESOT wameona umuhimu wa kutoa elimu kwa waganga na tayari wamekuwa na mafunzo  ambayo yameratibiwa na chama hicho kwa kushirikiana na mamlaka za serikali hususani wizara ya Afya, Tamisemi, chuo cha Sayansi shirikishi DIAHAS  Milembe na wengineo, mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa awamu mikoa mbalimbali yanawajenga waganga kutoa tiba salama, kufuata kanuni na taratibu ikiwemo kujasiliwa, kutokujihusisha na imani za kishirikina na mengine mengi, pia washiriki hupatiwa vyeti sambamba na Leseni kutoka mamlaka za serikali.

Hata hivyo amezitaja changamoto katika mafunzo hayo ikiwemo ushirikiano mdogo kutoka kwa watendaji wa kata, vijiji, mitaa na baadhi ya waratibu ambao wamekuwa sehemu ya upotoshaji juu ya mafunzo hayo ambapo changamoto hiyo ameitaja kujitokeza mara dhaa wilaya ya Misingwi mkoani Mwanza jambo ambalo ameliweka wazi kuwa moja ya sababu yenye kudhoofisha jitihada za mafunzo hayo hivyo ameiomba serikali kupitia wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala kuwashirikisha watendaji hao kutoa ushirikiano badala ya kuwa vikwazo dhidi ya zoezi hilo.
Mbali na hayo amewasisitiza waganga kuuona umuhimu na kuchukua hatua ya kujifunza ili kuwawezesha kutumikia tiba yenye mabadiliko makubwa yakitaalamu na kuachana na dhana ya tiba ya kienyeji kama ilivyozoeleka, ambapo amewasihi wananchi kutibiwa na wataalamu wenye sifa na vigezo ili kuepukana na kutapeliwa na watu wanaotumia mwavuli wa tiba asili matokeo yake kusababisha madhara kwa jamii yakiwemo mauaji.
Aidha amehitimisha akiishukuru serikali kupitia mamlaka za juu kwa namna zinavyotoa ushirikiano wakutosha ili kufanikisha mafunzo hayo muhimu ambayo yanaendelea maeneo mbalimbali yaliyonzia mkoani Dodoma.
