Jeshi la Polisi Mkoani wa Kilimanjaro linamshikilia mtu mmoja aitwaye Beatrice Gabriel Urassa (59) kwa tuhuma za mauaji ya watu wanne ambao walifariki dunia kwa nyakati tofauti wakiwa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Machame na hospitali ya Wilaya ya Hai.
Akizungumza kuhusu kukamatwa kwa mtu huyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa amewataja waliofariki dunia ni Hamida Hamis Kweka (26), Robson Edson Meena (34), Ismail Exaud Uronu (34) na Kamama Exaud Uronu (45) wote wakazi wa kitongoji cha kinyaro, kata ya Mnadani, wilaya ya Hai na Mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa, mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwapatia dawa za kienyeji watu hao ambao ni ndugu wa familia moja, na kupelekea kufariki dunia wakiwa wanapatiwa matibabu Julai 05, 2026 majira ya usiku.
Kamanda Maigwa amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusina na tukio hilo na pindi utakapokamilika taratibu nyingine za kisheria zitafuata.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mnadani, Emanuel Mgonja, amesema msiba huo ni pigo kubwa kwa kata hiyo na kuwataka wananchi kuendelea kushikamana, kusaidiana na kuifariji familia iliyoathirika.
Baadhi ya ndugu wa karibu wa marehemu walieleza kuwa vifo hivyo vilitokea ghafla na katika mazingira yasiyo ya kawaida, wakidai kuwa marehemu hawakuwa na historia ya kuugua kabla ya kuanza kuzidiwa kwa nyakati tofauti ndani ya kipindi kifupi.
Kwa mujibu wa maelezo yao, mwanzo walizidiwa mke na mume, baadaye Ismail Uronu naye akazidiwa, huku siku iliyofuata Rose Kweka naye akiugua na hatimaye kufariki dunia na kwamba Ndugu mwingine wa familia hiyo bado anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kimashuku ameiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia watoto walioachwa na marehemu, akieleza kuwa miongoni mwao yupo mtoto mwenye umri wa miezi saba huku familia ikiwa haina uwezo wa kuwahudumia ipasavyo.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Mnadani, Sembuli Mkilaa, ametoa wito kwa wananchi wa kata hiyo na jamii kwa ujumla kuepuka matumizi ya dawa na vinywaji ambavyo havijathibitishwa na mamlaka husika ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika.
