Benki ya Dunia imeitaka Serikali ya Kenya kuharakisha upitishaji wa Sheria ya Kulinda Watoa Taarifa (Whistleblower Protection Bill), ikieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi na kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za umma.
Muswada huo, ambao umekwama kwa miaka kadhaa, ni miongoni mwa masharti yaliyowekwa chini ya kifurushi kipya cha mkopo wa dola za Marekani Milioni 750 kwa nchi hiyo, kilichoidhinishwa mwishoni mwa Juni mwaka huu.
Mbali na sheria hiyo, Benki ya Dunia imeitaka Kenya kutekeleza mageuzi mengine muhimu, ikiwemo kuimarisha sheria za kuzuia mgongano wa maslahi kwa viongozi wa umma, kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa manunuzi ya serikali na kuweka akaunti moja ya Hazina ili kuboresha usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Kenya, Qimiao Fan, kila fedha inayopotea kutokana na rushwa na mifumo dhaifu ya usimamizi ni hasara kwa huduma muhimu kama elimu, afya na miundombinu.
Benki hiyo imeeleza kuwa maandamano ya mwaka 2024 yaliyotokana na ongezeko la kodi yalionesha wazi kuwa Wananchi wanataka uwajibikaji na usimamizi wa haki wa fedha za umma.
Aidha, pamoja na uchumi wa Kenya kukua kwa asilimia 4.6, nchi hiyo bado inakabiliwa na deni kubwa la umma, ukosefu wa ajira katika sekta rasmi na kupanda kwa gharama za maisha, huku ongezeko la bei za mafuta na vyakula kutokana na vita vya Mashariki ya Kati likikadiriwa kuwasukuma takribani watu Milioni moja zaidi kuingia kwenye umaskini.