Kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimejadili na kulaani kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, ya kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini, ikisema kuwa zuio hilo ni haramu na linakiuka ibara mbalimbali za Katiba (18, 20, 26, na 29) zinazotoa haki ya kujieleza na kujumuika.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Julai 10, 2026, katika Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam juu ya maazimio ya kikao hicho yaliyofanyika mkoani Kigoma Juni 30, 2026, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika ameeleza kuwa si Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri Mkuu, wala Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mwenye mamlaka ya kikatiba ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa.
Mbali na kutaka zuio hilo liondolewe mara moja na wale wote waliohusika wawajibishwe, CHADEMA imeunga mkono jitihada za kisheria zinazochukuliwa na wadau wengine dhidi ya zuio hilo na kuwasihi Watanzania wasikubali kupigishwa magoti na kile ilichokiita utawala usioheshimu demokrasia.
“Aidha kamati kuu pamoja na kulani zuio hiyo inaunga mkono jitihada za kisheria zilizofanywa na zinazokusudiwa kuchukuliwa na wadau wengine wa haki na utawala wa sheria nchini dhidi ya zuio hilo haramu. Kamati Kuu inawaahidi kila msaada wa kimawazo na ushahidi katika mapambano yao”, ameeleza Mnyika.
Katika hatua nyiingine, Kamati Kuu ya CHADEMA imeridhishwa na mafanikio makubwa ya operesheni ya “Katiba Mpya Free Tundulissu”, ikiwashukuru Watanzania kwa kuunga mkono chama tangu kilipofunguliwa kutoka kwenye zuio la kisiasa la Juni 2025 na kwamba Kamati imeazimia kuendeleza operesheni hiyo kwa nguvu katika kanda za Pwani, Unguja, na Pemba, na baadaye katika mikoa yote ya Tanzania