Latest Posts

TUHUMA UBADHIRIFU WA MALI ZA CHAMA ZALETA MPASUKO CHADEMA: VIGOGO WAWILI WAWEKWA KANDO, HECHE AHUSISHWA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaelezwa kuwa kwenye kiza cha mtafaruku baina ya viongozi wakuu, chanzo kikidaiwa kuwa ni fedha ambazo zimeanza kupenyezwa ndani ya chama hicho ili kuuvuruga na ikiwezekana kuuondoa uongozi wa juu uliopo (Mwenyekiti Tundu Lissu na Makamu Mwenyekiti Bara John Heche).

Kwa muda wa wiki moja tangu vikao vya kamati kuu ya chama hicho vikaliwe Kigoma Juni 30, 2026 zimeenea taarifa kwenye mitandao ya kijamii juu ya tuhuma dhidi ya Heche kudaiwa kupewa mamilioni ya fedha ambazo ni michango ya wadau kusaidia shughuli za chama hicho lakini kiongozi huyo hakuzikabidhi kwenye chama bali alibaki nazo.

Katika madai hayo yaliendelea kueleza kuwa kiongozi huyo alikiri kufanya hivyo na Kamati Kuu iliazimia kutolitoa jambo hilo nje badala yake waridhiane ndani kwa ndani na kujiponya.

Hata hivyo siku za karibuni zimeibuka tuhuma mpya dhidi ya Heche kuwa anashirikiana na wafanyabiashara kwa lengo la kuvuruga biashara ya mafuta nchini. Tuhuma hizi zimetolewa na kada wa chama hicho Lembrus Mchome na watu wengine.

Upepo umebadilika siku nne zilizopita ambapo inadaiwa kuwa tuhuma hizi ni za kumchafua Heche na zinaendeshwa na makada wa chama hicho wakishirikiana na watu wengine ikidaiwa kuwa wanaoendesha propaganda hizi walilipwa fedha kwa lengo la kwenda kushawishi kwenye kamati kuu ili Heche akubali kuingia kwenye maridhiano na serikali na Tundu Lissu aachiwe jambo ambalo inadaiwa Heche alikataa.

Tuhuma hizi zimekuwa zikimuelekea Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho Godbless Lema, Boniface Jacob na Joseph Mbilinyi, ‘Sugu’.

Wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA hawakukaa kimya juu ya hili, wamekuwa wakiandika taarifa zenye utata ambapo Mwenyekiti wa BAVICHA Wakili Deogratius Mahinyila aliandika “CHADEMA ni Lissu&Heche ndio waliokabidhiwa jahazi, tutawalinda kwa wivu mkubwa…tukilinde chama hiki na viongozi wake puuzeni umbea”

Naye Godbless Lema usiku wa kuamkia leo ameandika andiko lenye utata akisema, “iwapo italazimu kutetea heshima yangu binafsi dhidi ya kauli mbalimbali za dharau na upotoshaji nitafanya hivyo kwa ufasaha”.

Mwanaharakati Mange Kimambi naye hakuwa nyuma kulizungumzia suala hili. Ameandika kupitia machapisho yake kwenye mtandao wa X, “Heche anapigwa vita sababu kuna viongozi ndani ya CHADEMA wamefika bei ya maridhiano na CCM, Kwahiyo wanajaribu kumuondoa Heche ili waweke mtu ambaye atafanya maridhiano…Huu mpango wa kumuondoa kama kiongozi wa Chadema kupitia kumchafua kuwa kaiba pesa za tonetone”.

‎Katikati ya sintofahamu hii, CHADEMA Kanda ya kaskazini kimewasimamisha katika nyadhifa zao viongozi wawili ambao ni Katibu wa chama hicho Jimbo la Bumbuli, Abubakar Mashambo, na Joseph Mwakidasi wa Wilaya ya Muheza kwa tuhuma za kukiuka kanuni za maadili ya viongozi wa chama.

‎Kwa mujibu wa taarifa ya Julai 8, 2026 iliyotolewa na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Yohana Kaunya, uamuzi huo umefikiwa ikiwa ni baada ya viongozi hao kuchukua uamuzi wa kutoa tamko mbele ya vyombo vya habari dhidi ya Makamu Mwenyekiti, Heche bila kufuata utaratibu. Taarifa hiyo imesema tuhuma zilizotolewa dhidi ya Makamu Mwenyekiti hazina uthibitisho bali zimelenga zaidi kuchafua heshima ya kiongozi huyo.

‎”Kwa mujibu wa ibara ya 6.3.6(c) ya Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006, toleo la 2019, ametakiwa kuwasilisha uthibitisho wa tuhuma hizo ndani ya siku 14 tangu kupokea taarifa rasmi ya tuhuma” imeeleza taarifa hiyo ikisisitiza kuwa kusimamishwa kwa viongozi hao kumefuata utaratibu wa kisheria na kutadumu hadi kamati tendaji ya kanda husika itakapoketi ili kutoa uamuzi wa mwisho kwa mujibu wa sheria.

Haya yote yamekuwa yakiacha maswali mengi kwa wanachama wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla, ambapo Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA Brenda Rupia amesema maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho yatatangazwa hivi karibuni.

“Ajenda ni mbili Uhuru wa Mwenyekiti Tundu Lissu na Katiba mpya tusiache ajenda hizi zipotezwe na mijadala ya pembeni” ameandika Brenda kupitia ukurasa wake wa X.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!