
Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imetakiwa kuisimamia ipasavyo Taasisi hiyo na kuishirikisha sekta binafsi ili kufikia malengo ya Taifa yaliyokusudiwa katika sekta ya Utalii.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na Wajumbe Bodi hiyo Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanya tathmini, kushauri na kuboresha ili kuiwezesha TTB kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa ili kufikia malengo ya kuwa na watalii milioni nane ifikapo 2030 ni lazima Sekta binafsi ishirikishwe ipasavyo ili kukuza utalii na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa.
“Tushirikishe sekta binafsi ili tuweze kufikia malengo. Hata jumbe tunazozipeleka kwenye masoko tuwashirikishe sekta binafsi ili tuweze kufanikiwa kufikisha watalii milioni 8 na zaidi ifikapo mwaka 2030. Sekta binafsi iwe sehemu ya maisha yetu ya kila siku,” amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, ameitaka Bodi hiyo kuweka malengo yanayopimika yatakayowezesha kutathmini utendaji wake na kuongeza ufanisi katika kufikia azma ya Serikali ya kuongeza idadi ya watalii nchini.
Pia, amesisitiza umuhimu wa TTB kuendelea kufanya tafiti na kufuatilia mwenendo wa masoko mbalimbali ya utalii duniani ili kubaini mahitaji ya watalii na kuishauri Serikali pamoja na taasisi zake kuhusu maboresho yanayohitajika.
“Sisi ndio tuliopewa jukumu la kuiuza nchi huko nje, hivyo tunapaswa kuzishauri taasisi nyingine kuhusu mahitaji ya soko la kimataifa. Kwa mfano, TFS na taasisi nyingine zinapaswa kufahamu kwa wakati mahitaji ya watalii ili ziweze kuboresha huduma na bidhaa za utalii,” amesema.
Akizungumzia matukio makubwa yanayotarajiwa kufanyika nchini, ikiwemo AFCON na Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Kijaji ameitaka Bodi ya Utalii kuhakikisha inajiandaa kikamilifu kutumia matukio hayo kama fursa ya kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya utalii katika masoko ya kimataifa.
“Tunayo matukio kadhaa makubwa yanayokuja mbele yetu. Tujipange vya kutosha kabla ya matukio hayo ili tuyatumie kama fursa ya kuitangaza Tanzania na kuongeza idadi ya watalii,” amesema.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji taasisi zote kupanga na kutekeleza mikakati kwa pamoja ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB, Mhe. Balozi Dkt. Ramadhani Kitwana Dau, amesema Bodi hiyo imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha inafikia malengo ya Serikali katika sekta ya utalii. Amesisitiza kuwa moja ya malengo makuu ni kufikisha idadi ya watalii zaidi ya milioni 8 ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuvuka lengo lililowekwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Kikao hicho cha Dkt. Kijaji na Bodi ya Wakurugenzi ya TTB kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hassan Abbas, Mkurugenzi wa Utawala, Benard Marcelline; Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dkt. Theresa Mugobi, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Emmanuel Buhohela, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru; pamoja na wajumbe wa Bodi hiyo.