Tanzania imetoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa ili kuhakikisha maendeleo ya kasi ya Akili Unde (AI) yanasimamiwa kupitia mifumo iliyo jumuishi, yenye uwazi na usawa, huku ikisisitiza kuwa nchi zinazoendelea hazipaswi kuachwa nyuma katika mapinduzi ya teknolojia hiyo.
‎Akizungumza katika Mdahalo wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Akili Unde (Global Dialogue on AI Governance), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki (Mb), alisema Tanzania inaiona Akili Unde kuwa nyenzo muhimu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kukuza uchumi wa kidijitali.

‎Alisema Serikali inaendelea kuboresha sera na mifumo ya udhibiti ili kuhimiza ubunifu, kulinda haki za wananchi na kuhakikisha matumizi ya Akili Unde yanakuwa salama, yenye uwajibikaji na yanawanufaisha Watanzania wote.
‎”Tanzania inaamini kuwa Akili Unde ina uwezo wa kuleta mageuzi makubwa katika sekta za kilimo, afya, elimu, huduma za kifedha na utawala wa umma, hivyo, matumizi yake yanapaswa kuwa salama, jumuishi na kuhakikisha wananchi wote wananufaika,” alisema Waziri Kairuki.
‎Alieleza kuwa Serikali inaandaa mifumo ya udhibiti wa Akili Unde, ikiimarisha usimamizi wa data, ulinzi wa faragha na usalama wa mtandao, pamoja na kuandaa miongozo ya matumizi ya teknolojia hiyo katika sekta za kimkakati, zikiwemo elimu na afya.
‎
‎Kwa upande wa miundombinu, Waziri alisema Serikali inaendelea kupanua Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na kuendeleza Miundombinu ya Umma ya Kidijitali (Digital Public Infrastructure – DPI), hatua zinazolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali na kuwezesha matumizi mapana ya Akili Unde nchini.
‎Mhe. Kairuki pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kujenga mifumo madhubuti ya utawala wa Akili Unde. Alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU), Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuimarisha mifumo ya kidijitali inayowezesha ubunifu, biashara na huduma za kuvuka mipaka huku ikilinda usalama wa data.
‎Akihitimisha hotuba yake, Waziri huyo alitoa wito wa kuongezwa kwa ushirikiano katika uhamishaji wa teknolojia, maendeleo ya ujuzi, tafiti, ubunifu na uwekezaji katika miundombinu ya kidijitali ili kuziba pengo la kidijitali na kuhakikisha manufaa ya Akili Unde yanawanufaisha kwa usawa wananchi wa nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
‎
‎Mdahalo huo wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Akili Unde umewakutanisha watunga sera, viongozi wa serikali, wataalamu wa teknolojia na wadau wa sekta binafsi kutoka mataifa mbalimbali kujadili namna ya kujenga mifumo ya kimataifa ya kusimamia Akili Unde na kuongeza mchango wake katika maendeleo jumuishi na endelevu.