Na Amani Hamisi Mjege na Merina Makasi.
Kulikucha mapema tarehe 31 Agosti, anga la Dodoma likiwa safi na barabara ya kuelekea Morogoro ikiwa wazi kama kawaida, hakuna ambaye alifahamu kuwa siku hii ingesimulia hadithi ya huzuni ambayo ingewaacha wengi wakiwa na masikitiko makubwa.
Katika eneo la Manchali, Wilaya ya Chamwino, ukimya ulikatishwa ghafla na mlipuko wa ajali mbaya. Gari aina ya Costa, likiwa na abiria waliokuwa wakitoka njia ya Dodoma kuelekea Morogoro, lilijikuta likikabiliana uso kwa uso na lori aina ya Scania, lililokuwa limebeba mafuta ya petrol na likielekea Dodoma.
Katika muda upatao majira ya saa 12 asubuhi, maisha ya watu wanne yalikatishwa ghafla. Dereva wa Costa na abiria wawili walipoteza maisha papo hapo, huku mmoja wa majeruhi akifariki dunia akiwa hospitalini.
Ajali hii iliacha majina 16 zaidi katika orodha ya majeruhi, wakihangaika na maumivu ya miili yao na mshtuko wa kisaikolojia kutokana na tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la abiria aina ya Costa.
“Tumefika hapa kwenye eneo la tukio, ambapo ajali hii imetokea tarehe 31 Agosti majira ya saa 12 asubuhi, katika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro. Magari mawili, Costa ya abiria na lori aina ya Scania lililokuwa limebeba mafuta ya petrol, yamegongana uso kwa uso,” amesema Kamanda Katabazi.
Amefafanua ajali hiyo imetokea baada ya dereva wa Costa kushindwa kuchukua tahadhari wakati akijaribu kulipita gari jingine mbele yake, na kusababisha kugongana uso kwa uso na lori.
“Barabara ipo wazi, haina kona. Dereva wa Costa angechukua tahadhari, ajali hii ingeweza kuepukika,” amesema kwa masikitiko.
Huku hayo yakiendelea, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ilikuwa na pilikapilika nyingi. Daktari Florence Ramson, kutoka kitengo cha magonjwa ya dharula alieleza jinsi walivyopokea majeruhi 13, ambao wengi wao walipewa huduma ya kwanza mara tu walipofikishwa hospitalini.
“Wengi wanaendelea vizuri isipokuwa wagonjwa watatu ambao walipelekwa moja kwa moja chumba cha upasuaji kutokana na mivunjiko. Pia, tunao mgonjwa mmoja na mtoto walioko ICU,” alisema Dkt. Ramson akieleza hali ya wagonjwa hao.
Miongoni mwa majeruhi hao ni Abdallah Salehe, ambaye alikumbuka kwa uchungu safari yao ya kutoka Kahama mkoani Shinyanga kuelekea Dar es Salaam. Walikuwa safarini kama familia iliyokuwa ikisherehekea harusi ya ndugu yao.
“Dereva wa lori alikosea njia, akatukabili uso kwa uso na hapo ajali ikatokea,” alisema Abdalaah, sauti yake ikitetemeka kwa maumivu na huzuni.
Kwa upande mwingine, Ester Steven, mkazi wa Dar es Salaam, alikuwa na kisa tofauti. Hakukumbuka kilichotokea, kwani alikuwa amesinzia na alishtuka tu baada ya ajali kutokea.
Huku ajali hii ikiacha nyoyo nyingi zikiwa na maumivu, Kamanda Katabazi amesisitiza dhamira ya Jeshi la Polisi kuzuia matukio kama haya kutokea tena. Ameahidi kuimarisha doria na kuhakikisha kuwa sheria za usalama barabarani zinaheshimiwa ili maisha ya watu wasio na hatia yaendelee kuwa salama.
Lakini kwa familia na marafiki waliopoteza wapendwa wao, maumivu ya siku hiyo yatabaki kuwa kumbukumbu isiyofutika, simulizi ya huzuni iliyosukwa kwenye barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.