Latest Posts

AFYA YA KINYWA: MAONESHO MAKUBWA YA MENO KUFANYIKA DAR

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa wito kwa wadau wa afya na wananchi kutumia maonesho ya Tanzania Dental Expo 2026 kama jukwaa la kupambana na hali ya kuoza meno nchini, ambayo sasa inawaathiri zaidi ya asilimia 76 ya watu wazima.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam leo jijini hapa, DC Mpogolo amesema kuwa maboresho makubwa yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya lazima yaende sanjari na kupungua kwa magonjwa yanayozuilika kama kuoza kwa meno na maumivu ya fizi.

 

DC Mpogolo amebainisha kuwa serikali haiwezi kufurahia ujenzi wa vituo vya afya na ongezeko la vifaa tiba ikiwa takwimu za wagonjwa wa meno zinaendelea kupanda. Amesisitiza kuwa maonesho yatakayofanyika tarehe 28 mpaka 30 Mei, 2026 katika ukumbi wa Mlimani City, ni fursa ya kipekee ya kutoa elimu na huduma za kisasa.

“Sasa sisi watu wazima, haya meno yetu sasa, meno ya ukubwa, tunaita permanent teeth, kwa mtu yeyote ambaye ameanza kuotesha meno ya utu uzima kuanzia miaka sita (6) mpaka mia moja (100) na kuendelea, kiwango chetu ambacho kinatakiwa kuwepo kwenye dawa za meno ni elfu moja mia nne hamsini (1450) mpaka elfu moja mia tano (1500) PPM ya fluoride”, ameonya Dkt. Nzobo.

Mkuu huyo wa wilaya amepongeza uongozi wa Tanzania Dental Expo kwa kutafsiri kwa vitendo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050. Amefafanua kuwa dira hiyo inalenga kuona sekta binafsi ikishika zaidi ya asilimia 70 ya uchumi wa nchi ifikapo mwaka 2050, na maonesho hayo yanadhihirisha jinsi sekta binafsi inavyoweza kuongoza katika kuleta wawekezaji na teknolojia mpya nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya maonesho hayo, ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Afya ya Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Baraka Nzobo, amesema takwimu hizo ni kubwa kuliko ugonjwa mwingine wowote nchini, huku watoto wakionekana kuathirika kwa asilimia 31.8.

Dkt. Nzobo amebainisha kuwa sababu kubwa inayosababisha watu wazima kuendelea kuoza meno ni matumizi yasiyo sahihi ya dawa za meno. Amefafanua kuwa watu wazima wengi wanatumia dawa zenye kiwango kidogo cha fluoride (1000 PPM), ambacho ni maalum kwa watoto wa miaka 0 mpaka 5.

“Sasa sisi watu wazima, haya meno yetu sasa, meno ya ukubwa, tunaita permanent teeth, kwa mtu yeyote ambaye ameanza kuotesha meno ya utu uzima kuanzia miaka sita (6) mpaka mia moja (100) na kuendelea, kiwango chetu ambacho kinatakiwa kuwepo kwenye dawa za meno ni elfu moja mia nne hamsini (1450) mpaka elfu moja mia tano (1500) PPM ya fluoride”, ameonya Dkt. Nzobo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Clara Mwamba, amethibitisha kuwa TanTrade itaendelea kuunga mkono maonesho hayo kwani yanatoa jukwaa kwa wazalishaji wa ndani kukutana na wadau wa nje na kubadilishana uzoefu wa kiteknolojia.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Dental Expo, Frank Mwakatobe, alibainisha kuwa maonyesho hayo yanalenga kukuza uwekezaji katika sekta ya afya, kupunguza rufaa za wagonjwa wanaotafuta matibabu ya kibobezi ya meno nje ya nchi, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kutoa elimu kwa umma na kuunga mkono ajenda ya serikali ya kutoa huduma za afya kwa wote (Universal Health Coverage).

Maonesho haya yanatarajiwa kukutanisha wadau zaidi ya 2,000 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo watengenezaji wa vifaa vya meno, vyuo vikuu, na makampuni ya bima. Mwakatobe amewahimiza wananchi kuhudhuria kwani kiingilio ni bure na kutakuwa na fursa ya kupata habari, huduma, na uvumbuzi mpya katika afya ya kinywa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!