Latest Posts

SHERIA YA WATU WENYE ULEMAVU YATAJWA KULETA MABADILIKO CHANYA KWA JAMII

Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za makusudi kuhakikisha watu wenye ulemavu, hususan wenye Down Syndrome, wanapata haki, huduma na fursa sawa na wananchi wengine.

‎Hatua hizo ni pamoja na kuwepo kwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sura 183, ambayo inalinda na kutetea haki za watu wenye ulemavu katika nyanja zote za maisha.

‎Hayo yameelezwa leo Jumatano, Machi 25, 2026, jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu, Kizito Lukas Wambura, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Down Syndrome yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro, yenye kaulimbiu ya mwaka huu: “Tuwe pamoja dhidi ya upweke.”

‎Wambura amesema serikali inatambua kuwa watu wenye Down Syndrome wana haki sawa na wengine katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

‎Ameeleza kuwa jamii ya watu wenye Down Syndrome ina nafasi muhimu katika maendeleo ya taifa kupitia elimu, sanaa, ujuzi wa kazi, michezo, pamoja na mchango wao katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa kitamaduni. Amesisitiza kuwa ushirikishwaji wao kikamilifu utaongeza tija, ubunifu na mshikamano wa kijamii, na hivyo kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

‎Aidha, serikali imeendelea kuwezesha wanafunzi wenye ulemavu, ikiwemo wenye Down Syndrome, kusoma pamoja na wenzao kupitia shule jumuishi, vitengo maalum na shule maalum kulingana na mahitaji yao.

‎Pia, serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, wakiwemo mashirika ya kiraia na ya kimataifa, katika kubuni na kutekeleza miradi ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa watu wenye ulemavu.

‎Kila mwaka, tarehe 21 Machi huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Down Syndrome. Mwaka 2011, Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio la kuitambua rasmi siku hiyo, ikiwa ni fursa kwa mataifa kutafakari mchango na nafasi ya watu wenye Down Syndrome katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!