Watu sita wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watu watatu katika matukio mawili tofauti yanayotajwa kuwa ni kulipiza kisasi katika kijiji cha Ilabilo wilayani Kakonko mkoani Kigoma.
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Evance Malasa amemueleza mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuwa katika tukio la kwanza mtoto wa miaka mitano (5) mwenye ulemavu wa miguu na mikono aliyefahamika kwa jina la Simioni Furaha, alipotea Alhamis ya tarehe 18 Julai, 2024 na mwili wake kukutwa siku ya Jumamosi ya tarehe 20 Julai, 2024 ukiwa umefukiwa katika kichaka jirani na makazi ya watu kijijini hapo huku ukiwa na ishara ya kunyongwa.
Kanali Malasa amesema, kufuatia tukio hilo wananchi wenye hasira walimvamia Stephano Ndagwe ambaye nyumba yake ipo jirani na eneo ulipokutwa mwili wa mlemavu huyo na kuanza kumshambulia kwa vitu vyenye ncha kali na kusababisha kifo chake sambamba na kuchoma moto nyumba na kukata mazao yake ya shambani wakimuhusisha na tukio hilo.
Amebainisha kuwa baada ya tukio hilo, wananchi hao wakaendelea kuwatafuta watu wengine wanaoishi katika nyumba ya marehemu Stephano na kumkamata mtoto wa wake aliyetambuliwa kwa jina Alfayo Stephano (14) aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Kabingo na kumuua kwa kumchoma moto kwa kile wananchodai kuangamiza kizazi cha watu katili katika kijiji hiko.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Adengenye Julai 20, 2024 ametembelea wilayani humo na kuwasihi wananchi wa kijiji hiko kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kuwataka watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwabaini watuhumiwa wa matukio hayo na kuwafikisha mahakamani.
Aidha, Andengenye amesema, serikali haiwezi kukubali kuvumilia vitendo vya aina hiyo na kamwe haitawaacha salama watu wanaotaka kuweka mazingira hatarishi kwa wengine na kusisitiza kuwa hatua kali zitachukuli dhidi ya wahusika ili matukio ya aina hiyo yasiweze kujirudia.
Mpaka sasa tayari watu sita wamekamatwa kijijini hapo kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo huku jeshi la polisi likiendelea na upepelezi zaidi kuhusu tukio hilo.