Kamanda wa Jeshi la Polisi Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amewahakikishia Wananchi kuwa Jeshi la Polisi halilali na limekuwa likifanya doria maeneo yote, nchi kavu na majini na hata mtandaoni kupitia wataalamu wake wa makosa ya mtandao. Alibainisha kuwa tayari kuna watumiaji wa mitandao hiyo ambapo wapo wahalifu ambao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa ya mtandaoni
”Wapo ambao tumekua tukiwakamata kwa makosa mbalimbali ikiwemo makosa ya wizi wapo ambao wameshitakiwa na wapo ambao wamefikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Kamanda Mutafungwa alisema kuwa hakuna mhalifu wa mtandaoni aliye salama kwani sheria ipo wazi na inaeleza utaratibu mzuri wa kuwashughulikia na kuwachukulia hatua wale wanaofanya uhalifu huo, huku akitoa wito kwa wananchi kuacha tabia hiyo kwani jeshi la polisi lipo makini kuhakikisha doria zinafanyika kwa weledi mkubwa.
Hayo aliyasema alipokuwa akijibu ombi la katibu wa Usafirishaji (bodaboda) Thomas Michael kwenye mkutano wa kusikiliza kero za wananchi Kata ya Usagara wilaya ya Misungwi baada ya boda huyo kuomba Serikali kudhibiti mitandao ya kijamii inayozua taharuki na kuwa kichocheo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili kwani Vijana wamekuwa wakisambaza habari potofu za uchochezi zinazozua taharuki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Misungwi Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Gasper Silayo aliwasitiza wananchi kuendelea kutunza na kudumisha amani ili kila mwananchi aweze kufanya shughuli zake kwa usalama na kujiingizia kipato.
Naye Diwani wa Kata ya Usagara Erasto Kashinje akatumia nafasi yake kwa niaba ya wananchi kuomba radhi kwa tukio lililotokea la kuchomwa moto kituo cha polisi Nyashishi katika vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025.

Kashinje aliongeza kuwa kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kumalizia ujenzi wa kituo kipya cha polisi Usagara chenye hadhi ya Daraja “C” kilichopo kata ya Usagara wilayani humo ili kurejesha huduma za usalama karibu na wananchi.

Janeth Evalista, mkazi wa Nyashishi yeye ameomba uwepo wa kituo cha polisi cha dhalula katika kata hiyo kufatia Vijana wengi kujiingiza kwenye kamali na unywaji pombe kiasi cha kujiuliza wanatoa wapi pesa za kunywea pombe na kucheza kamali.