Latest Posts

ORYX ENERGIES YAZINDUA KITABU CHA MAFUNZO YA LPG KUIMARISHA MATUMIZI SALAMA YA GESI NCHINI

 

Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Ltd, Benoit Araman amesema kampuni hiyo imeendelea kutekeleza wajibu wake wa kijamii kwa kuwekeza katika elimu ya matumizi salama ya gesi ya kupikia (LPG), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati hiyo kwa usalama.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha mwongozo wa mafunzo ya LPG, Benoit amesema lengo la Oryx si tu kufanya biashara bali pia kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha maisha ya wananchi kupitia elimu na uhamasishaji wa matumizi salama ya gesi.

Amesema wananchi ndio wadau muhimu zaidi kwa kampuni hiyo, hivyo Oryx imeamua kuwekeza katika mipango itakayosaidia kutoa elimu kwa jamii nzima kuanzia mijini hadi maeneo ya vijijini kuhusu matumizi sahihi ya LPG.

“Ukitaka kwenda haraka nenda peke yako, lakini ukitaka kwenda mbali nenda pamoja. Kwa nchi kubwa kama Tanzania yenye mamilioni ya watumiaji wa gesi, tunahitaji ushirikiano ili kufikisha elimu ya matumizi salama ya LPG kwa kila mwananchi,” amesema Benoit.

Ameeleza kuwa ushirikiano na Chama cha Skauti Tanzania utakuwa chachu muhimu katika kufikisha mafunzo hayo kwa jamii mbalimbali, ambapo skauti watafundishwa na baadaye kuwaelimisha watumiaji wa mwisho wa gesi katika maeneo tofauti nchini.

Amesema kitabu hicho ni nyenzo ya kujifunzia itakayosaidia kutoa elimu kuhusu usalama wa matumizi ya LPG, huku akisisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa matumizi ya gesi.

Kwa upande wake Mtunzi wa kitabu hicho, Peter Ndomba amesema wazo la kuandaa mwongozo huo lilitokana na maono ya Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania na uzoefu mkubwa wa kampuni hiyo katika sekta ya gesi.

Amesema maudhui ya kitabu hicho yameandaliwa kwa kushirikisha uzoefu wa Oryx pamoja na maarifa kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa ya LPG (World LPG Association), ambayo kampuni hiyo ni mwanachama na kupata utaalamu pamoja na nyenzo mbalimbali za kiufundi.

“Tunataka watu wawe salama, kwa sababu mtu ambaye hajapata mafunzo ya matumizi ya gesi bado hayuko salama. Kitabu hiki kitasaidia kutoa elimu ya gesi, matumizi salama ya gesi na miongozo inayotakiwa kuzingatiwa,” amesema Ndomba.

Ameongeza kuwa kitabu hicho ni cha kwanza kutolewa na kampuni ya gesi nchini kwa ajili ya kuwawezesha watumiaji wa bidhaa zake kupata elimu sahihi, na kitapatikana kwa mfumo wa karatasi pamoja na kidijitali.

Naye Ofisa Rasilimali Watu wa Oryx Gas Tanzania, Lilian Mwakagile amesema uzinduzi wa kitabu hicho ni mafanikio makubwa katika tasnia ya mafuta na gesi nchini, kwa kuwa kitakuwa mwongozo muhimu kwa watumiaji wa bidhaa za kampuni hiyo.

Amesema kitabu hicho kitasaidia wananchi kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo usalama wa matumizi ya LPG, matumizi sahihi ya nishati safi na namna ya kuhakikisha familia na jamii zinakuwa salama.

“Ni kitabu ambacho kinaweza kutumika nyumbani na familia, watoto, wazazi pamoja na jamii kwa ujumla kwa sababu kinatoa elimu muhimu kuhusu matumizi salama ya gesi,” amesema Mwakagile.

Akizungumza katika hafla hiyo, Skauti Mkuu wa Tanzania, Lt. Rashid Mchatta ameipongeza Oryx Gas Tanzania kwa kuwa miongoni mwa waanzilishi wa uwekezaji katika sekta ya LPG nchini, akisema ushirikiano huo utaongeza nguvu katika kutoa elimu kwa jamii.

Amesema mwaka uliopita Skauti Tanzania ilianza kushirikiana na Oryx kupitia mafunzo yaliyofanyika Dodoma ambapo kwa mara ya kwanza skauti walitumia majiko ya gesi katika kambi zao kwa msaada wa kampuni hiyo.

Ameeleza kuwa hatua iliyofikiwa sasa ni muhimu zaidi kwa kuwa skauti watatumika kama waelimishaji wa jamii katika kuhakikisha wananchi wanapata maarifa ya matumizi bora na salama ya gesi.

“Skauti tuna uzoefu katika kutoa elimu kwa jamii na tutafanya kazi hii kwa bidii kuhakikisha tunafikia malengo na kutoa matokeo chanya,” amesema Lt. Mchatta.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!