Jeshi la Polisi nchini limewaonya waganga wa tiba asili na tiba mbadala wanaojihusisha na vitendo vinavyokiuka sheria, ikiwemo kutoa ramri za uchonganishi zinazochochea migogoro kati ya ndugu na jamaa na kuhatarisha amani, ulinzi na usalama wa nchi.
‎Onyo hilo limetolewa na Kamishna wa Polisi Jamii kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kamishna Alex Mkama, alipokuwa akizungumza na waganga wa tiba asili na tiba mbadala waliokutana Kibaigwa, wilayani Kongwa mkoani Dodoma kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wadau wa sekta hiyo pamoja na kuwakumbusha wajibu wao wa kuzingatia sheria za nchi.
‎Katika hatua nyingine, Kamishna Mkama amewakumbusha waganga hao kuzingatia sheria na taratibu za nchi katika utekelezaji wa majukumu yao, akionya dhidi ya matumizi ya nyara za serikali bila kibali au kufuata utaratibu unaotakiwa.
‎Awali, Mratibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kutoka Wizara ya Afya, Dk. Mussa Mpukuta, amesema ushirikiano kati ya serikali na wadau wa tiba asili ni muhimu katika kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kuzingatia sheria, maadili na usalama wa wananchi.
‎Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala (TAMESO T ), Bujukano Mahungu, amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha wanachama wake wanazingatia sheria na kufanya kazi kwa weledi.