Jumla ya vijana 200 kutoka Jimbo la Geita Mjini wamehitimu mafunzo ya udereva wa pikipiki, baada ya kufanya mitihani na kukabidhiwa leseni, kupitia ufadhili wa Mbunge wa jimbo hilo, Mhandisi Chacha Wambura.
Mafunzo hayo yaliyochukua takribani wiki mbili, yalihusisha wakufunzi kutoka Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Chato pamoja na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge, Msaidizi wa Mbunge, Mduma Chambua, aliwasisitiza wahitimu hao kuzingatia mafunzo waliyoyapata ili kuimarisha usalama barabarani na kuepuka ajali zisizo za lazima.

Kwa upande wake, Inspekta Gabriel Rweikiza, akimwakilisha RTO wa Mkoa wa Geita, aliwataka madereva hao kuwa mfano bora kwa wengine kwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.
Naye Mwenyekiti wa waendesha pikipiki mkoani humo, Fred Fidel, alimshukuru Mbunge Wambura kwa kugharamia mafunzo hayo, akieleza kuwa yamewasaidia vijana wengi kujiajiri kupitia shughuli ya bodaboda.