Latest Posts

“TUPIGE KELELE KUKATAA UKATILI WA KIJINSIA”- MAHUNDI

 

‎Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa malezi kwa kuwajenga watoto katika maadili mema na kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoathiri watoto na wanawake.

‎Amesema malezi bora ni msingi wa kujenga jamii yenye maadili na kwamba kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama yanayowawezesha kuwa raia wema na wenye mchango kwa Taifa.



‎Mahundi ametoa kauli hiyo alipokuwa akifanya ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo katika Wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma.

‎”Tupige kelele kukataa ukatili wa kijinsia na tuwalinde watoto wetu ili wakue katika mazingira salama yatakayowafanya kuwa raia wema na wenye mchango kwa Taifa,” amesema.

‎Katika ziara hiyo, Mahundi pia amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kusimamia na kuendeleza miradi ya kiuchumi inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuongeza kipato, kuinua ustawi wa familia na kuchochea maendeleo ya jamii.



‎Amesema serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi mbalimbali kupitia mikopo, mafunzo na miradi ya maendeleo, hivyo wananchi wanapaswa kuitunza na kuisimamia ili ilete tija ya kudumu.

‎Katika ziara hiyo, ametembelea Kikundi cha Wanawake Ubihumwe kilichopo Kata ya Gwarama, Kikundi cha Vijana Tuinuane na Shule ya Msingi Itumbike yenye kitengo cha watoto wenye mahitaji maalum. Pia alikutana na kikundi cha watu wenye ulemavu cha Kakonko na kuzindua jengo la kivuli cha Soko la Kijiji cha Kanyonza.



‎Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kakonko, Allan Mvano, amesema ataendelea kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha miradi inayotekelezwa jimboni humo inaleta matokeo chanya katika sekta za elimu, uwezeshaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na kuboresha huduma za kijamii.

 

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!