Latest Posts

MADAI YA RUSHWA, MPIRA WETU TUNAUZIKA WENYEWE

Na; mwandishi wetu

Rushwa michezoni, ni miongoni mwa mambo yaliyopewa katazo na kuwekewa adhabu kali sana ulimwenguni kote, hiyo inaenda sambamba na uwepo wa matendo ya udanganyifu na upangaji wa matokeo, matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kwa wanamichezo nk, vyote hivyo ni miongoni mwa mambo yaliyopigwa marufuku karibu na mashirikisho ya michezo yote Duniani

Kwa upande wa mpira wa miguu kama ilivyokuwa kwa michezo mingine, na ikizingatiwa kuwa huo ni mchezo pendwa namba moja Duniani sheria imekuwa kali sana, hapa mamlaka za soka ulimwengu zikiongozwa na Shirikisho la soka Duniani (FIFA) limeenda mbali zaidi kwa kueweka sheria na adhabu kali sana kwa serikali zitakazoingilia maamuzi ya mpira wa miguu

Hapa ieleweke wazi kuwa, haijapigwa marufuku serikali kusaidia au kushiriki kwenye shughuli za michezo hususani mpira wa miguu la hasha, ila kilichopigwa marufuku ni serikali kujiingiza kwenye kufanya maamuzi ya masuala ya soka, adhabu ya jambo hilo endapo ikibainika ni pamoja na Taifa husika kufungwa kujihusisha na masuala ya Soka, kama ilivyo kwa nchi ya Congo kwa sasa

Ndio maana sio dhambi kwa serikali kulipa mishahara, posho nk kwa wachezaji au makocha wa klabu au timu za Taifa kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kusaidia ukuaji wa michezo kwenye nchi husika, na ni ukweli usiopingika kuwa ni ngumu kwa vyama vya michezo kuendesha shughuli zake bila kuwa na ushirikiano thabiti na mamlaka za kiserikali, hata hivyo endapo ikatokea kuna mashauri na sintofahamu imejitokeza kwenye mpira wa miguu kwa mfano na inahitajika kufanyiwa maamuzi basi hapo umewekwa utaratibu mahsusi kuanzia ngazi za chini hadi FIFA, na katu katika hilo imepigwa marufuku ‘mpira kupelekwa Mahakamani’

Pamoja na yote hayo, lakini inapotokea masuala ya Rushwa au viashiria vyake, basi moja kwa moja licha ya kwamba mamlaka za mpira zinaweza kuchukua hatua zake lakini pia si dhambi kwa vyombo vya kiserikali, na kwamba Tanzania mfano TAKUKURU au ZAECA kuingilia kati na kushughulika na wale wanaohisiwa kujihusisha kupokea au kutoa rushwa kwa namna moja au nyingine

Hivi karibuni golikipa Patrick Matasi wa klabu ya Kakamega Home Boys ya kule nchini Kenya, na mchezaji wa timu ya Taifa hilo (Harambee Stars) amefungiwa kujihusisha na mpira kwa muda wa siku 90 huku shirikisho la soka nchini Kenya (FKF), shirikisho la soka barani Afrika (CAF) na FIFA wakiendelea na uchunguzi kabambe dhidi yake kuhusiana na tuhuma za upangaji wa matokeo ya michezo mbalimbali inayohusisha klabu yake na timu ya Taifa

Matasi aliingia kwenye ‘mkenge’ huo baada ya video zake kusambaa mitandaoni akionekana na kusikika kama anajadiliana na mtu mmoja (ambaye hakufahamika mara moja) kuhusu dau la endapo kwenye mchezo fulani utatoa GG (watu wanaojihusisha na michezo ya ubashiri watakuwa wamenielewa vizuri hapa), na yeye kuahidiwa donge nono la pesa endapo angefanya hivyo, na inadaiwa kuwa mchezo husika ulitoa GG kama ilivyokusudiwa, ikumbukwe kuwa haya yote yalitokea katika wakati ambao Matasi amekuwa akisifika kuwa na kiwango bora sana na kabla ya mchezo huo uliotoa GG timu yake ilikuwa haijawahi kuruhusu bao kwa mechi nne (4) mfululizo

Hapa Tanzania, sitaki kusema kama tuko salama sana dhidi ya tuhuma za rushwa, na upangaji wa matokeo michezoni hususani mchezo wa mpira wa miguu, nasema hatuko salama salama sana sio tu kwa sababu sisi sio kisiwa bali kwa muda mrefu, na kwa miaka mingi kumekuwa na tuhuma za aina hiyo zimekuwa zikitajwa kwenye mpira wetu, bahati mbaya sana ni kwamba kama yanayosemwa yana uhalisia basi hakuna mtu yeyote aliyewahi kujitokeza hadharani kutoa ushahidi wa wazi utakaopelekea wadaiwa kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu, na kama hakuna ushahidi basi zinaendelea kubaki kuwa ni tuhuma na kelele tu za kishabiki

Hata hivyo, tutakuwa wajinga sana kama tuhuma na kelele hizi tutaendelea kuzikalia kimya bila kuanza kuchukua hatua hata ya kufanya uchunguzi wa kimyakimya ili kujuwa ukweli wake, kwa maana haiwezekani miaka yote kelele ni hizohizo tu na hazifiki tamati (leo kwa timu X, kesho kwa timu Y, kesho kutwa kwa kiongozi Z, mtondogoo kwa mchezaji nk) ni lazima tuchukue hatua kama Taifa, na kama hazina uhalisia basi tuchukue hatua kali kwa wale wanaosambaza uzushi huo, maana tukikaa kimya tunahalalisha haramu na kuutia doa mpira wetu, maana kwenye hili wanaochafuliwa sio viongozi, makocha, na wachezaji pekee bali mamlaka za mpira za nchi husika na hata serikali nayo inachafuliwa, tuchukue hatua kali za haraka na makusudi

Tuna mifano mingi sana,  lakini kwa wakati huu naomba niiweke mifano miwili hapa, wa kwanza ni ule unaotokana na sakata la kuhairishwa kwa mchezo wa Yanga SC na Simba SC, mchezo uliotarajiwa kufanyika Machi 08 mwaka huu, sasa ajenda yangu hapa si kusimulia ‘songombingo’ zote hadi kuhairishwa kwake, hayo ni ya wakati mwingine na pengine tumeyasema na kuyasikia sana, ajenda yangu ni taarifa ya kuhairishwa kwa mchezo huo ya Bodi ya Ligi (TPLB) iliyotolewa mchana wa siku hiyo, ikiwa ni saa chache kabla ya muda wa mchezo

Yalielezwa mengi kwenye taarifa ile lakini TPLB imesema miongoni mwa sababu ilizopelekea kuhairishwa kwa mchezo husika ni uwepo wa viashiria vya rushwa kuelekea mchezo husika, ingawa taarifa hiyo haikufafanua kwa kina kama viashiria hivyo vinawahusu nani na nani haswa, lakini kuwepo kwa neno ‘Rushwa’ ni jambo ambalo linapaswa kupokelewa kwa uzito mkubwa sana, ingawa walitoa taarifa hiyo lakini ilinishangaza kusikia kuwa taarifa hizo hazijafikishwa kwenye vyombo mahsusi vya kushughulikia masuala ya rushwa kama vile TAKUKURU, hadi sasa najiuliza kama kulikuwa na viashiria vya rushwa sasa anayechunguza ni nan?, na katika hili tuwaombe mamlaka za soka nchini hususani TFF/TPLB kutofanya mambo gizani, badala yake kila kitu kiwekwe kwa uwazi hata kama kinawagusa mabwana au mabibi wakubwa, kukaa kimya ni kuendelea kuutia doa mpira wetu, na hii haikubaliki

Mfano wangu wa pili unahusiana na mchezo wa Tabora United dhidi ya Yanga SC, mchezo unaotarajiwa kupigwa leo, Jumatano Aprili 02.2025 kwenye dimba la Ally Hassan Mwinyi, mkoani Tabora, kila mmoja atakubaliana na mimi kuwa kuelekea mchezo huu kuna ‘vimbwanga’ vingi sana tumeviona na kuvisikia, tambo na shamra shamra hizo hatuna shida nazo, tatizo ni pale tunaposikia na kuona kauli zinazoashiria masuala ya rushwa na upangaji wa matokeo kuelekea mchezo huo, na kwa bahati mbaya sana, narudia tena kwa bahati mbaya sana baadhi ya kauli hizo zinatolewa na viongozi wenye mamlaka makubwa tu serikalini

Mfano, kuelekea mchezo huo Mkuu wa mkoa wa Tabora Paul Chacha amenukuliwa akisema hivi, “wapo wanaowadanganya najuwa, na wengine wanapitisha meseji, nyie achaneni nao, hela chukueni ila fanyeni kazi yenu, na niwahaidi dhidi ya Simba SC niliweka milioni 50 ila sasa ni milioni 60 kwa sababu nafahamu Yanga SC watakuja na viherehere”

Hiyo ni kauli ya Mkuu wa mkoa, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa na kiongozi mwandamizi serikalini, lakini ikumbukwe huyu ni mteule wa Rais, sitaki kuamini kwamba kaongea haya kwa bahati mbaya, nashawishika kuamini kuwa huenda kuna jambo nyuma ya pazia linaendelea hadi kumsukuma kusema yote hayo

Hata hivyo nimeshangazwa kusikia anasema ‘hela chukueni ila fanyeni kazi yenu’, kwa lugha rahisi hapa anaharalisha rushwa, sheria inasema anayetoa na kupokea wote wana makosa, halafu kwa nini asitumie nafasi yake kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kwa mkoa wake hususani TAKUKURU kuingia kati badala yake anawaambia wachezaji ‘chukueni’, au tuseme alikuwa anafanya utani sio?, ndio labda alikuwa hamaanishi, lakini kwani Tabora United na Yanga SC ni watani?, Paul Chacha na Yanga SC ni watani?, Paul Chacha na wachezaji wa Tabora United ni watani?, hili linafikirisha

Kubwa kuliko yote, hivi sasa kuna saut inayotembea kwa kasi sana kwenye mitandao ya kijamii, inadaiwa kuwa sauti hiyo ni ya Andy Lobuka Bikoko (golikipa wa Tabora United), inasikika akizungumza na mtu mmoja (ambaye hajafahamika mara moja) lakini kwa aina ya maongezi ni kama vile ‘katumwa’ kutoka Yanga SC ili amshawishi yeye (Bikoko) aruhusu Yanga SC ashinde mechi, tunaendelea kufuatilia hili tujuwe mwarobaini wake

Hadi sasa hakuna uthibitisho wa moja kwa moja lakini kama mambo haya yana uhalisia, ukijumlisha na makandokando yetu kwenye mpira hapa nchini nathubutu kusema kuwa mpira wetu ‘tunauzika’ wenyewe.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!