Serikali imewahakikishia wapenzi na mashabiki wa soka nchini kuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa haujafungwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), huku ikibainisha kuwa ukarabati wake umekamilika na uko tayari kwa matumizi.
Akizungumza Jumatano, Machi 12, 2025, jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa, amesema kuwa taarifa za kufungiwa kwa uwanja huo zinatokana na ukaguzi wa CAF uliofanyika wiki tatu zilizopita, baada ya mechi kati ya Azam na Simba Februari 24, 2025.
“CAF walitaka uwanja huu uboreshwe zaidi, hasa eneo la kuchezea (pitch), na walihitaji kuona mashine maalum za kurekebisha uwanja, ambazo kwa wakati huo zilikuwa njiani kutoka China. Lakini kwa sasa uwanja uko tayari,” alisema Msigwa.
Serikali Yaiagiza TFF Kuwasiliana na CAF
Msigwa ameongeza kuwa Serikali imeiagiza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwasiliana na CAF ili shirikisho hilo lifanye ukaguzi mpya wa uwanja huo, kwa kuwa maboresho yote yaliyohitajika tayari yamefanyika.
“CAF walipaswa kututaarifu kabla ya kutoa taarifa hizi. Sasa tumeshaelekeza TFF wawasiliane nao ili waje kufanya ukaguzi wao upya,” alisema.
Hatma ya Mechi ya Yanga na Simba
Kuhusu mechi ya Yanga dhidi ya Simba iliyopangwa kuchezwa Machi 8, 2025, lakini ikaahirishwa, Msigwa amesema kuwa Serikali haina mamlaka ya kuingilia suala hilo, na kwamba TFF na Bodi ya Ligi ndio wanaopaswa kutoa majibu.
“Waulizeni TFF, siyo Serikali, wao ndio wana bodi ya ligi. Hata sisi tulipanga kuitumia mechi hiyo kuzindua ushirikiano kati ya TFF na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini ikaahirishwa,” alifafanua Msigwa.
Amehitimisha kwa kusema kuwa kwa sasa Uwanja wa Benjamin Mkapa uko tayari kwa mechi yoyote, na CAF wanaweza kuja kufanya ukaguzi muda wowote.