Latest Posts

‘DEMOKRASIA NI ZAIDI YA UCHAGUZI’: BALOZI TINNES AZITAKA NCHI KUIMARISHA TAASISI NA UTAWALA WA SHERIA

Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes, amesema kuwa demokrasia si lengo lililokamilika mara moja bali ni mchakato endelevu unaohitaji kufanywa upya na kudumishwa na kila kizazi.

Kauli hiyo imetolewa leo, Septemba 15, 2026, mkoani Dar es Salaam wakati Balozi Tinnes akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Demokrasia Duniani yaliyoratibiwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Balozi Tinnes amebainisha kuwa ingawa demokrasia inakabiliwa na changamoto kubwa duniani kote, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa uaminifu wa umma na kubana kwa nafasi za kiraia barani Ulaya na Afrika Mashariki, tafiti za kimataifa zinaonesha kuwa watu wengi barani Afrika bado wanapendelea demokrasia kuliko mifumo ya kiimla.

Ameongeza kuwa matukio ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na yaliyofuata nchini Tanzania yanakumbusha kuwa demokrasia haiwezi kuchukuliwa kama jambo lililojipata lenyewe bila kuilinda na kuiimarisha.

Akizungumzia misingi mikuu inayowezesha demokrasia kuwa imara, Balozi Tinnes amesema, “demokrasia imejengwa kwa muda na kudumishwa kupitia kujitolea kwa mwendelezo… Kwanza, taratibu za kidemokrasia lazima ziwe za wazi, zenye kuaminika na za haki. Pili, demokrasia inahitaji ushindani halisi wa kisiasa na ushiriki wenye maana. Watu lazima wawe huru kueleza mitazamo tofauti, kujipanga kwa amani na kushiriki katika mijadala ya umma bila hofu”.

Akiendelea kufafanua, mwanadiplomasia huyo ameeleza kuwa ustahimilivu wa demokrasia unategemea kuwepo kwa utawala wa sheria ambapo sheria inatendeka kwa usawa kwa wananchi wote bila ubaguzi. Amesisitiza kuwa utawala wa sheria ndio unaobadili misingi ya kidemokrasia kuwa vitendo vinavyolinda haki za raia na kuwezesha walio madarakani kuwajibishwa

“Demokrasia ni zaidi ya uchaguzi pekee. Inategemea taasisi imara, mgawanyo wa wazi wa madaraka na ulinzi unaodumisha uwazi, uwajibikaji na ushindani wa haki wa kisiasa. Utawala wa sheria unabadilisha misingi ya kidemokrasia kuwa vitendo, unalinda haki, na kuhakikisha wale wanaotekeleza madaraka wanaweza kuwajibishwa”, ameongeza Balozi Tinnes.

Aidha, Balozi Tinnes ameeleza kuwa sheria na taasisi pekee hazitoshi bila kuwepo kwa mashirika huru ya kiraia yanayofanya kazi ya kusikiliza wananchi, kutetea haki, na kuhimiza uwajibikaji. Amepongeza jitihada za muda mrefu za LHRC nchini Tanzania katika kutetea haki za binadamu, upatikanaji wa haki, na mabadiliko ya kisheria, akibainisha kuwa Norway inajivunia ushirikiano wake wa muda mrefu na kituo hicho

“Katika kuadhimisha Siku ya Demokrasia Duniani, tukumbuke kwamba demokrasia haijawahi kukamilika mara moja na kwa wote. Sio lengo, ni mchakato… Kupitia mazungumzo ya wazi, kuheshimu haki za binadamu, taasisi imara na mashirika ya kiraia yanayofanya kazi, Tanzania na Norway zinaweza kuendelea kujenga demokrasia jumuishi, inayowajibika na yenye ustahimilivu”, ameeleza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!