Latest Posts

e-ARDHI KULETA MAGEUZI MAKUBWA KATIKA HUDUMA ZA ARDHI

 

Mfumo wa e-Ardhi umeelezwa kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za ardhi kwa wananchi wa Mkoa wa Singida, kwa kupunguza misongamano, mizunguko na muda mrefu wa kufuatilia huduma katika ofisi za ardhi.

Kupitia mfumo huo wa kidijiti, wananchi watapata huduma mbalimbali za ardhi kwa njia ya mtandao, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

Akizungumza Septemba 14, 2026 mkoani Singida wakati wa mafunzo matumizi ya mfumo huo pamoja na namna wananchi watakavyonufaika nao, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Bi. Shamim Hoza, amesema mfumo huo utasaidia kuboresha kwa kiasi kikubwa utoaji huduma za ardhi katika mkoa huo.

Bi. Hoza amebainisha kuwa, mfumo wa e- Ardhi utapunguza msongamano wa wananchi katika ofisi za ardhi, kuondoa mizunguko isiyo ya lazima ya kufuatilia huduma na kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma.

“Mfumo huu utaongeza uwazi na kupunguza msongamano usio wa lazima katika ofisi zetu,” amesema Bi. Hoza.

Aidha, Kamishna Hoza amewataka wataalamu wa ardhi katika Mkoa wa Singida kuwa tayari kuupokea na kuutumia mfumo huo, akieleza kuwa ni miongoni mwa hatua muhimu zitakazoleta mageuzi makubwa katika utoaji huduma bora kwa wananchi.

 

Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Ibrahim Magessa, amesema mfumo huo ni mzuri na utarahisisha upatikanaji huduma kwa wananchi, hususan katika kuomba nyaraka mbalimbali za ardhi, ikiwemo hati.

Naye Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Singida, Koletha Timanywa, ameeleza kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwao kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kwa kasi.

Kwa mujibu wa Timanywa, ni jukumu la wataalamu hao kuhakikisha wanauelewa na kuumudu mfumo huo ili kuboresha zaidi huduma wanazowapatia wananchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!