Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Camillus Wambura, tarehe 4 Septemba, 2026, amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Kipolisi wa Rufiji na kukutana na viongozi wa Kijiji cha Jaribu Mpakani, Kata ya Mjawa, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali yanayohusu hali ya usalama na ustawi wa eneo hilo.
Katika mazungumzo hayo, IGP Wambura amewatoa hofu wakazi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani, akiwataka kuendelea na shughuli zao za kila siku za kiuchumi na kijamii kwa kuwa hali ya usalama nchini ni shwari na imara wakati wote.

Pamoja na kutoa wito huo wa kimaendeleo, IGP Wambura amesisitiza umuhimu wa jamii kuimarisha malezi bora na maadili kwa watoto ili kujenga kizazi chenye uzalendo kinachotambua na kuthamini amani ya nchi.
Ziara hiyo imelenga pia kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Jeshi hilo, ikiwemo Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa na vituo mbalimbali vya polisi. Katika ukaguzi huo, IGP Wambura ameambatana na viongozi waandamu wa Jeshi la Polisi, akiwemo Kamishna wa Fedha na Lojistiki, CP Liberatus Sabas; Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai; na Kamishna wa Utawala na Rasilimaliwatu, CP Tatu Jumbe.
Akitathmini uwekezaji huo wa miundombinu, IGP Wambura ameeleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuthamini juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa rasilimali fedha na vifaa, ambavyo vinasaidia kurahisisha utendaji wa kazi za kila siku na kuongeza ufanisi katika kulinda raia na mali zao.