Latest Posts

NDEJEMBI AAGIZA KUSAWAZISHA MNYORORO WA UZALISHAJI ILI SIMENTI ISHUKE BEI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ametoa agizo kwa Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanamaliza haraka mkwamo wa uzalishaji unaosababisha bei ya saruji kupanda na kumuumiza mwananchi wa kawaida.

Akizungumza jana Jumatano, Septemba 2, 2026, alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika msimu wa 19 wa Tuzo za Rais za Wazalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA) jijini Dar es Salaam, Ndejembi alionesha kusikitishwa na gharama kubwa ya mfuko wa saruji inayomkabili Mtanzania hivi sasa.

“Sasa nakuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara namwona hapa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kaeni pamoja mmalize hili suala ili Mtanzania apate saruji kwa bei iliyokuwepo. Nataka kupata ripoti ya suala hilo baada ya kikao hiki, mjadili na mwandike ripoti tumkabidhi Rais,” alisisitiza Ndejembi.

Alifafanua kuwa changamoto kubwa inasababishwa na kutokuwa na uwiano katika mnyororo mzima wa uzalishaji kati ya viwanda vinavyozalisha klinka (clinker) na vile vinavyosaga saruji (grinders).

Makamu wa Rais alieleza kuwa kukosekana kwa uwiano huo kunasababisha baadhi ya wasagaji kukosa klinka ya kutosha kwa sababu mzalishaji mkubwa wa malighafi hiyo hazalishi ipasavyo, jambo linalopelekea uhifadhi au ukandamizaji wa bidhaa sokoni (holding of goods), na hatimaye mwananchi wa kawaida kuumia.

“Sisi kama serikali tunafanya nini katika kuhakikisha tunasynchronize production katika viwanda vyetu kwenye ile value chain yote?… Leo hii Mtanzania anapata gharama kubwa ya mfuko wa sementi. Ni kwa sababu hatuja-synchronize production yetu,” alisema Ndejembi.

Akiangazia mwenendo wa uchumi, Makamu wa Rais ameeleza kuwa sekta ya viwanda imeendelea kukua, ambapo mwaka 2025 ilikua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.2 ya mwaka 2024, huku mchango wake katika Pato la Taifa ukifikia asilimia 5.9 na kuchangia takribani asilimia 12 ya ajira rasmi nchini.

Hata hivyo, ametoa rai kwa wamiliki wa viwanda kutojiridhisha na soko la ndani pekee, bali kuongeza ubora na tija ili bidhaa za Tanzania ziweze kushindana katika masoko ya Afrika Mashariki na duniani kote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa CTI, Leodegar Tenga, ameeleza kuwa tuzo za PMAYA zinalenga kutambua mchango wa sekta ya viwanda na kuchochea ubunifu. Pia amesisitiza utekelezaji wa misingi ya uzalishaji endelevu unaozingatia mazingira, jamii na utawala bora (ESG), akitangaza kuanzishwa kwa Mabalozi 10 wa ESG watakaopimwa kwa mwaka mmoja.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!