Kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, inaendelea leo Jumatatu, Agosti 24, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Lissu ameendelea kushusha utetezi wake mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru, akieleza kwa kina historia ya harakati zake, mfululizo wa kesi alizofunguliwa wakati wa tawala tofauti, na uchambuzi wa kihistoria kuhusu kile alichokiita “uchafu” wa mfumo wa uchaguzi nchini.
Katika kuanza kwa ushahidi wake leo, Lissu ameiambia mahakama kuwa mara baada ya kesi hiyo kufunguliwa mwaka jana (2025), taasisi mbalimbali za kikanda na kimataifa zilitoa matamko makali ya kulaani mashtaka hayo. Taasisi hizo ziliziita tuhuma hizo kuwa ni za uonevu na matumizi mabaya ya mifumo ya mahakama na uendeshaji wa mashtaka ya jinai.
Miongoni mwa taasisi zilizotoa matamko hayo ni pamoja na Chama cha Mawakili wa Afrika Mashariki (EALS), Chama cha Wanasheria cha Nchi Wanachama wa SADC (SADCLA), Muungano wa Wanasheria Afrika (Pan African Lawyers Union – PALU), Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), pamoja na vyama vya mawakili vya Kenya na Zambia, Tume ya Wanasheria Duniani (ICJ) – Kenya Chapter, Ofisi ya Kikanda ya Amnesty International ya Afrika Mashariki na Kusini, Uganda Law Society (ULS), Democrats Union of Africa (DUA) na Platform of African Democrats (jukwaa linalounganisha vyama vya kidemokrasia vya nchi 17 barani Afrika).
Lissu amefafanua kuwa mnamo Julai 30, 2025, Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Haki za Wananchi (ACHPR) yenye makao makuu yake Arusha, ilifanya kikao cha dharura na kupitisha azimio rasmi lililoitaka Serikali ya Tanzania kuheshimu na kufuata mkataba wa Afrika wa haki za binadamu ulioridhiwa mwaka 1984.
Lissu ameeleza kuwa utetezi wake unathibitisha kwamba kesi hii si kwa sababu yeye ni mhaini, bali inatokana na msimamo wake wa miaka mingi wa kupigania haki na utawala bora. Alibainisha kuwa alianza harakati zake tangu akiwa shule ya sekondari mwaka 1988, ambapo alikaribia kufukuzwa shule kwa kuwatetea wanafunzi wa kidato cha nne wakati yeye akiwa kidato cha sita.
Mnamo mwaka 1989/1990, akiwa jeshini kama mtumishi katika kikosi namba 841KJ, mjadala wa kuanzishwa kwa vyama vingi ulipoanza, Lissu aligombana vikali na majenerali wa jeshi waliokuwa wanapinga mfumo huo. Alitumia kauli ya Mwalimu Julius Nyerere kuwa “wanaofikiri wanaotaka mabadiliko ni wajinga” kuwakabili viongozi hao wa jeshi. Aidha, Tume ya Nyalali ilipoundwa mnamo Februari 1991, Lissu alikuwa miongoni mwa Watanzania waliotoa ushuhuda mbele ya Jaji Mkuu wa zamani, Francis Nyalali, kutetea haja ya nchi kurudi kwenye mfumo wa vyama vingi.
Katika hatua nyingine, Lissu ameeleza kwa kirefu mchango wake katika kulinda rasilimali na haki za ardhi za wananchi wa kawaida ikiwamo kupigania haki za watu wa eneo la Ngorongoro. Amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za ardhi kule Loliondo, Tarime, Meatu, Maswa Mashariki, hifadhi za Serengeti, Pwani ya Kigoma, Nkasi, na maeneo ya mpaka wa Uganda ambako wananchi. Mwaka 2023, alikamatwa Karatu na kuzuiliwa katika kituo cha polisi Monduli ili asiende Ngorongoro kuwatetea Wamaasai.
Ameeleza kuwa tangu mwaka 1999, amekuwa akipigania haki za wachimbaji wadogo waliokuwa wakifukuzwa ‘kiholela’ kupisha wawekezaji wa nje. Baada ya kile alichokiita mauaji ya wachimbaji wadogo huko Bulyanhulu na serikali kupeleka majeshi kuwaondoa wananchi, Lissu na Dkt. Rugemeleza Nshala waliongoza kampeni ya kimataifa kudai uchunguzi huru, jambo lililowafanya wafunguliwa kesi yao ya kwanza ya jinai mwaka 2002. Katika eneo la Nzega na Tarime (Nyamongo), alipigania haki za wananchi na kufanikiwa kuwaondoa gerezani watu 466 waliokuwa wameshtakiwa kwa migogoro ya ardhi.
Lissu amejitambulisha kama kiongozi wa CHADEMA aliyeshtakiwa mara nyingi zaidi kuliko kiongozi yeyote, akitumia kauli mbiu ya, “Upinzani dhidi ya ukandamizaji ni utiifu kwa Mungu”. Ameieleza mahakama juu ya mfululizo wa kukamatwa kwake chini ya tawala tofauti ikiwamo ndani ya utawala wa Rais Mkapa, Kikwete, Magufuli na Samia.
Lissu ameeleza namna alivyokamatwa katika matukio tofauti wakati wa Uongozi wa Rais Samia mpaka sasa yupo gerezani akikumbusha tukio la Agosti 2024 (Mbeya) kuelekea siku ya Vijana Duniani, la Septemba 2024 kufuatia kutekwa na kuuawa kwa mjumbe wa CHADEMA, Ali Kibao, huko Ununio ambapo chama kilitangaza maandamano ya amani lakini asubuhi ya tarehe 23 Septemba nyumbani kwake, alikamatwa na akashikiliwa Central na kisha Mbweni kabla ya kuachiwa usiku bila mashtaka.
Tukio la mwisho ni la Aprili 9, 2025 ambapo likamatwa na kufunguliwa kesi hii ya sasa ya uhaini siku iliyofuata. Lissu amebainisha kuwa ameshakaa gerezani kwa takriban miezi 16 hadi 17, kipindi kirefu zaidi kuliko kiongozi yeyote wa kisiasa tangu kuanzishwa kwa vyama vingi.
Wakati wa utetezi wake, upande wa Jamhuri kupitia Wakili Katuga ulijaribu kuweka pingamizi ukidai kuwa maelezo ya Lissu kuhusu kukamatwa huko nyuma na vifo na mauaji ya viongozi na wanachama wa CHADEMA hayana umuhimu (irrelevant) kwenye kesi ya uhaini. Katuga pia alimshutumu Lissu kwa kusoma makarabrasha kinyume cha Kifungu cha 177 cha Sheria ya Ushahidi. Lissu alijibu kuwa sheria inamruhusu kurejea nyaraka ili kuamsha kumbukumbu, na akasisitiza kuwa kesi hiyo ni ya kutengenezwa na ya kisiasa, hivyo mfululizo huo wa matukio ni muhimu kuonesha kile alichokiita mfumo wa hila wa polisi na waendesha mashtaka.
Lissu amefafanua kuwa shtaka lake la uhaini linatokana na kauli yake ya tarehe 3 Aprili 2025 kuhusu uchaguzi mkuu. Alieleza kuwa upande wa mashtaka umewasilisha ushahidi wa video kutoka Jambo TV yenye urefu wa saa tatu, lakini maneno yanayodaiwa kuwa ni uhaini yakisomeka hayachukui hata dakika moja. Lissu amehoji: “Hayo masaa matatu niliyozungumza, nilizungumza kitu gani?”.
Akiingia kwenye uchambuzi wa kina wa kihistoria, Lissu ameeleza kuwa nchi imekuwa na mfumo mbovu wa uchaguzi tangu ukoloni:
Tume ya Nyalali (1991): Lissu amesema ilipendekeza kuwa na Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ifikapo Septemba 1993 kwa sababu mfumo uliopo ulikuwa wa chama kimoja na haukufaa kwenye demokrasia. Hata hivyo, Rais Ali Hassan Mwinyi alikataa mapendekezo hayo ili “kuokoa chama” (CCM).
Kudhibitiwa kwa Tume ya Uchaguzi (1992): Lissu amesema marekebisho ya sheria yalifanya wajumbe wote wa Tume kuteuliwa na Rais (ambaye ni mwana-CCM)
Mfululizo wa Migogoro ya Uchaguzi: Lissu amesema mfumo huu ulisababisha vurugu kubwa kwenye uchaguzi wa mwaka 1995 huko Dar es Salaam na Zanzibar ambapo vifaa vya uchaguzi vilicheleweshwa kwa hofu ya upinzani kushinda. Mapendekezo ya Tume ya Jaji Kisanga (1998) na Jaji Bomani (2003) ya kutaka Tume Huru yote yalikataliwa na Rais Mkapa. Vurugu za mwaka 2000 Zanzibar zilisababisha maafa na wananchi kukimbia nchi. Chini ya Kikwete, Tume ya Jaji Warioba (2014) ilijaribu kuleta katiba mpya lakini mchakato huo ulikwamishwa na CCM kwa mujibu wa Lissu.
Uchaguzi wa Mwaka 2020: Lissu ameeleza kuwa Sheria ya Uchaguzi inataka matokeo ya kura za Rais yachapishwe kwenye gazeti la serikali jimbo kwa jimbo. Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 hayajachapishwa hadi leo, na huenda makaratasi yote ya kura yamechomwa moto baada ya miezi sita kama sheria inavyoeleza, jambo linalofanya isijulikane kamwe Magufuli alipata kura ngapi.
Baada ya Lissu kumaliza kutoa sehemu hii ya utetezi wake uliodumu kwa masaa kadhaa, majaji wameahirisha kesi hiyo kwa muda ikitarajiwa kuendelea sa 8 na nusu mchana wa leo Agosti 24, 2026.