Latest Posts

DC MUFINDI AZITAKA NGOs KUWEKEZA KWENYE CHANGAMOTO HALISI ZA WANANCHI

 

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, amezitaka taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wilayani humo kuandika maandiko ya miradi yanayolenga kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi katika maeneo husika.

Dkt. Linda ametoa wito huo katika Jukwaa la Mwaka la Mashirika yasiyo ya Kiserikali wilayani Mufindi, lililofanyika katika Kata ya Mbalamaziwa, Wilaya ya Mufindi.

Amesema ni muhimu mashirika hayo kufanya tathmini ya mahitaji ya wananchi kabla ya kuandaa miradi, ili kuhakikisha rasilimali zinazopatikana zinatumika kutatua changamoto zenye uhitaji mkubwa.

Aidha, Dkt. Linda amesisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na mashirika hayo, akisema hatua hiyo itasaidia kuzuia miradi inayofanana kutekelezwa katika eneo moja wakati maeneo mengine yakiwa na uhitaji mkubwa.

Ametoa mfano wa miradi ya maji, akisema kuna wakati Serikali inapopeleka huduma hiyo katika kata fulani, shirika nalo hupeleka mradi wa maji katika eneo hilo hilo, badala ya kuelekeza nguvu katika eneo lenye uhitaji zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO) Fidelis Filipatali, amesema wameweka mikakati ya kuhakikisha hakuna kujirudia kwa miradi katika eneo moja huku akizitaka NGOs kuwa waaminifu katika matumizi ya misaada wanayoipokea ili iwafikie wananchi moja kwa moja na kuhakikisha miradi hiyo inalindwa kwa manufaa ya jamii.

Naye Mratibu wa World Vision Malangali na Idumbala, Zacharia Shigukulu, amezitaka NGOs kuzingatia miradi inayolinda maadili, mila na desturi za Tanzania huku wakihakikisha miradi wanayoitekeleza inaleta manufaa kwa jamii bila kuchochea mmomonyoko wa maadili.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!