Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, ametangaza kuwa chama chake hakiko tayari kuipigia magoti serikali kufuatia kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, na badala yake akawataka wanachama kuinua mapambano ya kidemokrasia nchini.
Akizungumza Ijumaa Agosti 21, 2026, katika Jengo la Edwin Mtei lililopo Makao Makuu ya CHADEMA mara baada ya kutoka mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi ya Lissu, Heche ameielezea siku hiyo kama “siku nyeusi” katika harakati za kupigania haki, lakini akasisitiza kuwa ni siku ya muhimu sana ya kuamsha na kuinua mapambano
Heche ametoa wito kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho kutoingia uoga; mikutano ya hadhara na vikao vya ndani viendelee, huku vijana wakiendeleza mapambano kwenye mitandao ya kijamii hadi ushindi utakapopatikana
Heche ameeleza kuwa mwenendo wa sasa wa serikali ni ishara ya uongozi unaoelekea mwisho ambao unazidi kujitengenezea maadui kila siku.
“Kila wanachokifanya wanaongeza maadui,” alisema Heche akitolea mfano wa kaka yake na Tundu Lissu, Mzee Alute Mughwai, ambaye ni mwanachama wa CCM lakini sasa analazimika kutafakari upya msimamo wake baada ya kuona mdogo wake akionewa na kudhulumiwa haki yake.
Alifananisha hatua za serikali na “mateke ya mwisho ya farasi anayekufa” au mtu anayezama kwenye mto akijaribu kushika kila jani na mti akiamini yatamuokoa, lakini mwishowe anazama
Kuhusu hali ya Mwenyekiti Tundu Lissu, Heche amewatoa hofu wanachama kwa kuthibitisha kuwa wamefanya naye mazungumzo na yuko imara kiakili na kisaikolojia
“Tumeongea na mwenyekiti wetu yuko katika hali ya juu sana ya morali (very high spirit), amejiandaa na yuko vizuri sana… atawatambaza kwa magoti,” alisisitiza Heche huku akiongeza kuwa hakuna kosa lolote lililofanyika na hivyo hawana hofu.
Makamu Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa ingawa uamuzi uliotokea Ijumaa umesikitisha, una umuhimu mkubwa wa kihistoria. Amesema kuwa vizazi vijavyo vitasoma kuhusu matukio haya na kwamba historia itawaweka viongozi na wanachama wa CHADEMA katika sehemu wanayostahili kwa kusimamia haki.