Serikali imeahidi kuendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili familia za viongozi wakuu wastaafu na wenza wao, ili kuhakikisha wanaishi kwa amani na usalama kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, ameyasema hayo wakati alipomtembelea Mama Fatuma Karume nyumbani kwake Unguja, Zanzibar, ambapo alimfikishia salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
’Niahidi nitakwenda kuwaelekeza watendaji katika ofisi yangu kushughulikia changamoto zinazojitokeza ili familia za viongozi na wenza hao ziendelee kuishi kwa amani na usalama, ” ameongeza Kikwete.
Amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anathamini mchango wa viongozi wakuu wa kitaifa waliomtangulia na ataendelea kusimamia na kutunza familia zao kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi.
Kwa upande wake, Mama Fatuma Karume amemshukuru Kikwete kwa kumtembelea na kumjulia hali, huku akimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijali familia yake.