Waziri Mkuu na Jaji mstaafu, Joseph Sinde Warioba, ameelezea kushangazwa na kuumizwa na wimbi jipya la ukamataji wa raia, wakiwemo wasomi, ambao wengine hufunguliwa mashtaka ya ugaidi mara tu wanapopata dhamana katika makosa ya awali.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na tovuti ya The Jenerali Ulimwengu Post kuhusu hali ya kisiasa nchini, Jaji Warioba amebainisha kuwa kuna mwelekeo wa mamlaka kutumia sheria za makosa yasiyo na dhamana kama nyenzo ya kutisha wananchi na kuwakosesha haki yao ya uhuru.
Jaji Warioba ametoa mfano wa kesi ya hivi karibuni mkoani Dodoma inayomhusu mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Melkisedeki Kaijage ambaye awali alishtakiwa kwa kosa la uchochezi ambalo kisheria lina dhamana. Alieleza kuwa baada ya mahakama kuridhia kumpa dhamana, mashtaka yalibadilishwa ghafla na kuwa ya ugaidi.
Kuhusu mchakato wa maridhiano ya kitaifa, Jaji Warioba ameonya kuwa matumizi ya mashtaka mazito kama ugaidi yanaweza kukwamisha juhudi za kuiponya nchi kufuatia yaliyotokea Oktoba 2025.
Aidha, Jaji Warioba, ametoa mtazamo wake wa kitaalamu na kisheria kuhusu hali ya kisiasa nchini, akionya kuwa ratiba ya serikali ya kupata Katiba Mpya ifikapo mwaka 2028 inaweza isiwe na tija kutokana na uhaba wa muda wa utekelezaji.
Amesema ingawa serikali inaonekana kukubali mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande ikiwemo kuundwa kwa Tume ya Maridhiano, bado kuna wasiwasi mkubwa ikiwa mchakato huo utahusisha wananchi kikamilifu.
Mapendekezo hayo yanalenga kukamilisha mchakato wa katiba ifikapo 2028 ili itumike katika uchaguzi wa serikali za mitaa (2029) na uchaguzi mkuu (2030). Hata hivyo amesema mnyororo wa matukio yanayopaswa kufuatwa kufikia kupatika kwa Katiba hiyo ni mrefu na mgumu.
Jaji Warioba amebainisha kuwa mchakato wa Katiba Mpya unahitaji hatua kadhaa nyeti, ikiwemo kazi ya kamati ya wataalam ya kulinganisha rasimu zilizopo, na muhimu zaidi, kukusanya maoni ya wananchi nchi nzima. Ameeleza kuwa kupata maoni ya wananchi si jambo la miezi mitano au sita, bali ni mchakato unaohitaji utulivu na muda wa kutosha ili kupata mwafaka wa kitaifa.