Serikali kupitia Wizara ya Nishati imetangaza mkakati thabiti wa kuhakikisha nchi inaondokana kabisa na changamoto ya kukatika kwa umeme nchi nzima, ikieleza kuwa lengo la sasa la wataalamu ni kuhakikisha nishati hiyo inakuwepo wakati wote bila adha ya nchi nzima kuingia gizani.
Mkakati huo umewekwa wazi leo Agosti 20, 2026, na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, wakati wa mahojiano maalum kuelekea uzinduzi wa kihistoria wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) utakaofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Jumamosi hii ya Agosti 22, 2026.

Akifafanua kuhusu hitilafu ya kiufundi iliyotokea mwezi Juni na kusababisha nchi nzima kukosa nishati hiyo, Mhandisi Luoga amesema kuwa changamoto hiyo ilikuwa ya kiufundi na imetafsiriwa kama fursa ya kuimarisha mifumo ya dharura ili kuzuia matukio ya aina hiyo kujirudia
“Kwa hiyo suala la kukatika umeme kwa nchi nzima, halitakiwi, halitakiwi. Kwahiyo imekuwa changamoto na fursa… huko tunakoelekea sasa tunataka tuondokane na hali ya kukatika kwa umeme kwa nchi nzima,” amesisitiza Mhandisi Luoga.
Ili kufikia azma hiyo, Wizara imeanza kutekeleza mipango madhubuti ikiwa ni pamoja na ujenzi wa njia huru na maalum ya kusafirisha umeme kwa ajili ya treni za mwendokasi (SGR) kuanzia Dar es Salaam hadi Makutopora, na tayari imeshafika Isaka na Mwanza. Hatua hii inalinda usafiri huo wa kimkakati na mtikisiko wowote wa gridi ya taifa
Pia, serikali imetenga kituo maalum cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi kilichopo Ubungo mkoani Dar es Salaam chenye uwezo wa takriban megawati 385 kama mbadala na ‘jenereta’ la dharura nchi nzima inapokabiliwa na changamoto ya nishati
“Endapo kutatokea na tatizo lolote pale bado tuna nafasi ya kuipatia umeme SGR, Na pamoja na mikakati tuliyokuwa nayo, mpango uliopo mwingine ni kuhakikisha kwamba kituo hicho hicho kinaweza kutumika kama jenereta hapo baadaye inapotokea tatizo lolote la umeme kwa nchi nzima basi baadhi ya maeneo yatakuwa yanapata umeme na SGR itakuwa inapata umeme,” amebainisha Kamishna Luoga