Latest Posts

ACT YAIBUKIA KUFUNGIWA KWA MWANAHALISI; YATAKA SHERIA YA HABARI YA 2016 IFUTWE

Chama cha ACT Wazalendo kimelaani uamuzi wa Idara ya Huduma za Habari (MAELEZO) wa kusitisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la MwanaHALISI kwa muda wa miezi sita, kuanzia tarehe 19 Agosti 2026.

Hatua hiyo ya Serikali imetokana na kile kilichodaiwa kuwa ni ukiukaji wa viwango vya usahihi na mizania katika toleo namba 571, ambapo gazeti hilo lilichapisha habari yenye kichwa “Nchimbi agoma kujiuzulu.” MAELEZO ilibaini makosa ya kiuhariri ikiwemo kuweka picha ya Waziri Paul Makonda na kumtaja kimakosa kama Makamu wa Rais wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, pamoja na kukosa uthibitisho kutoka kwa wahusika.

Kupitia taarifa rasmi kwa umma leo Agosti 19, 2026, Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo amesema kuwa ingawa wanatambua wajibu wa weledi, adhabu hiyo ni tishio kwa demokrasia.

“Serikali imejipa mamlaka ya kumchunguza, kumsikiliza na kumuadhibu mtoa huduma wa habari. Hii inakinzana na kanuni za haki na utawala bora,” amesisitiza Ayo.

ACT Wazalendo imetoa rai kuwa makosa ya kitaaluma yanapaswa kushughulikiwa kwa njia inayolinda uhuru wa habari na si kwa kufungia vyombo vya habari, jambo ambalo linagusa haki ya jamii kupata taarifa.

Kufuatia adhabu hiyo ambayo inajumuisha pia kuzuiliwa kwa maudhui ya gazeti hilo ya kielektroniki na mtandao, ACT Wazalendo imeitaka serikali isimamishe mara moja adhabu dhidi ya MwanaHALISI na kurejesha leseni yake, imetaka kufutwa kwa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na vifungu vyote inavyodai kuwa vinakandamiza uhuru wa habari na Kuundwa kwa chombo huru cha kitaaluma cha wanahabari cha kushughulikia malalamiko badala ya Serikali kuwa mlalamikaji na mwamuzi.

“Uhuru wa habari na haki ya kupata, kutoa na kupokea taarifa ni nguzo za Katiba, demokrasia na uwajibikaji wa Serikali. Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na sheria nyingine zinazoweka mamlaka makubwa Mkurugenzi wa Habari juu ya vyombo vya habari zinapaswa kufutwa”, ameeleza Ayo.

Licha ya adhabu hiyo kufuatia maonyo ya awali ya mdomo na maandishi yaliyotolewa mwezi Februari na Mei, gazeti la MwanaHALISI limepewa siku 30 kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya habari, utamaduni, sanaa na michezo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!