Latest Posts

TRUMP ATANGAZA “VITA VYA KIUCHUMI” DHIDI YA IRAN; AWEKA MKWARA MZITO KWA NCHI ZITAKAZOFANYA NAYO BIASHARA.

Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuanzisha vikwazo vipya na vikali vya kiuchumi dhidi ya Iran, huku akitoa onyo kali kwa nchi yoyote au taasisi itakayojihusisha na biashara au kutoa usaidizi kwa taifa hilo la Mashariki ya Kati.

Akitumia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Rais Trump ameeleza kuwa amechukua hatua hiyo kufuatia Iran kushindwa kufikia makubaliano ya kuzuia mzozo unaoendelea, baada ya muda wa makubaliano ya kusitisha vita kwa siku 60 kukamilika rasmi Jumatatu ya wiki hii bila kuwepo kwa dalili za amani.

Trump, ambaye mara kwa mara ametishia kuichukulia hatua kali zaidi Iran, amesema kuwa kuanzia sasa anatangaza operesheni kali zaidi ya kiuchumi kuwahi kuchukuliwa dhidi ya taifa lolote duniani, akifafanua kuwa yatakuwa ni “vita vya kiuchumi na kutengwa kiasi ambacho hakijawahi kushuhudiwa.”

Akiweka msimamo huo dhidi ya washirika wa Iran, Trump ametangaza kuwa nchi yoyote itakayoruhusu benki, taasisi za kifedha, kampuni za biashara, viwanja vya ndege, au asasi za kiserikali kuisaidia Iran, nayo itakabiliwa na adhabu na athari mbaya za kiuchumi kutoka Marekani.

“Marekani inatangaza vita vya kiuchumi visivyowahi kutokea. Nchi yoyote, benki, au chombo kitakachoamua kuisaidia au kufanya biashara na Iran, kitakutana na vipigo na athari mbaya sana za kiuchumi,” amesema Rais Trump.

Hata hivyo, Rais Trump hakutoa maelezo ya kina ya kiufundi kuhusu vikwazo hivyo vipya au kutaja majina ya mataifa yatakayolengwa mara moja. Kauli hii inakuja wiki moja tu baada ya Waziri wake wa Fedha, Scott Bessent, kusema kuwa Marekani inajipanga kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi visivyo na mfano.

Shinikizo hili jipya linalolenga uchumi wa Iran linakuja wakati vita hivyo vilivyoanzishwa mwishoni mwa mwezi Februari 2026 na Marekani ikishirikiana na Israel vikielekea kutimiza miezi sita bila uwepo wa jitihada thabiti za kidiplomasia.

Hatua hii ya Trump inatazamwa pia kupitia jicho la kisiasa la ndani ya Marekani, ambapo anachunguzwa kwa karibu kuelekea Uchaguzi wa Katikati ya Muhula (Midterm Elections) unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2026.

Naye mshirika wake, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, anakabiliwa na shinikizo kubwa la kisiasa kuhusu anavyomudu mzozo huo wa Iran na ule wa Gaza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Israel uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba 2026.

Licha ya mashambulizi ya makombora kupungua katika siku za hivi karibuni kati ya pande hizo, Iran imeendelea kuzuia usafiri wa meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz), ikiwa ni ishara ya mgogoro huo kuendelea kuathiri sekta ya nishati duniani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!