Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo tarehe 14 Agosti, 2026, saa 9.30 alasiri, limemkamata Wakili wa Kujitegemea, Peter Madeleka, akiwa katika eneo la Mikocheni B, Kinondoni. Madeleka amekamatwa akiwa katika viunga vya Mahakama ya Uhujumu Uchumi (maarufu kama Mahakama ya Mafisadi) wakati akitekeleza majukumu yake ya kitaaluma.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, Madeleka anashikiliwa na kuhojiwa kwa tuhuma za kudharau amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi iliyotolewa tarehe 27 Julai, 2026 na tarehe 13 Agosti, 2026.

“Lilimkamata na linamuhoji Peter Madeleka, kwa tuhuma za kudharau amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi “Mahakama ya Mafisadi” iliyotolewa tarehe 27 Julai, 2026 na 13 Agosti, 2026. Taratibu za kisheria zinatekelezwa ili kumfikisha kwenye mamlaka nyingine za kisheria kwa hatua zaidi”, imeeleza polisi.
Kukamatwa huku kumetokea saa chache baada ya Wakili Madeleka kufanya mkutano na waandishi wa habari akitangaza nia yake ya kufungua kesi kupinga zuio la Msajili wa Mahakama Kuu linalowazuia mawakili kufanya mahojiano na vyombo vya habari mahakamani. Taarifa za awali kutoka kwa Wakili Gideon Mathew zilieleza kuwa wakati wa ukamataji huo, watu waliojitambulisha kama polisi walichukua pia gari la Madeleka, fedha, na nyaraka mbalimbali alizokuwa nazo.
Aidha, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilieleza kupokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa kikitoa wito kwa mawakili waliopo Dar es Salaam na maeneo ya jirani kufika Kituo Kikuu cha Polisi (Central Police) ili kutoa msaada wa kisheria na kuhakikisha Wakili Madeleka anapata usaidizi unaostahili
“Chama cha Wanasheria Tanganyika kinaendelea kusimamia na kutetea haki, utu na uhuru wa mawakili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kitaaluma kwa mujibu wa sheria,” imeeleza taarifa ya TLS iliyotolewa na Baraza la Uongozi.