Waajiri ambao bado hawajajiunga na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), wametakiwa kuhakikisha wanajiunga na mfuko huo ili kuwawezesha wafanyakazi wao kupata fidia na huduma stahiki endapo watakumbwa na majanga au madhara yatokanayo na kazi.
Wito huo umetolewa mapema leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, wakati alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Mjini Geita.
Sangu amesema ni muhimu kwa waajiri kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kujiunga na WCF, kwa kuwa mfuko huo una jukumu la kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao pindi wanapopata ajali, kuugua au kukumbwa na madhara mengine yanayohusiana na shughuli za kazi.
Amesema uanachama wa WCF unatoa kinga kwa wafanyakazi na kuwawezesha kupata fidia pale wanapopata majanga yanayotokana na kazi, hivyo waajiri hawapaswi kusubiri hadi mfanyakazi apatwe na tatizo ndipo waanze kutafuta namna ya kumsaidia.
Waziri Sangu amesisitiza kuwa waajiri wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu zinazohusu ustawi na usalama wa wafanyakazi, akiwataka wale ambao bado hawajajiunga na mfuko huo kuchukua hatua mara moja ili kuhakikisha wafanyakazi wao wanalindwa.
Aidha, amewataka waajiri na wadau mbalimbali kutumia maonesho hayo kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na WCF, pamoja na kufahamu wajibu wao katika kuhakikisha wafanyakazi wanapata ulinzi na fidia wanapokumbwa na madhara yanayohusiana na kazi.
Kwa upande mwingine, wananchi na wadau wanaoshiriki maonesho hayo wamepata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu huduma za WCF, ikiwamo taratibu za kupata fidia na umuhimu wa mwajiri kutimiza wajibu wake wa kisheria kwa ajili ya usalama na ustawi wa wafanyakazi