Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, John Heche, amesema ni msimamo na sera rasmi ya chama hicho ya kuwalipa pensheni ya kila mwezi wananchi wote wanaofikisha umri wa miaka 60, kuwapatia huduma za matibabu ya daraja la kwanza (first class) bila malipo, pamoja na kuwekeza kwenye kilimo ili kulinda afya zao na usalama wa chakula nchini, pale chama hicho kitakapopewa nafasi ya kushika dola.
Heche ameyasema hayo tarehe 1 Oktoba 2026 wilayani Tarime, Mkoa wa Mara, wakati akizungumza kama mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Wazee la CHADEMA (BAZECHA).

Akiwahutubia wazee hao, Heche ameeleza kuwa wazee ndio waliojenga uchumi wa Tanzania kwa kukulima, kujenga nyumba, na kuzalisha mali, hivyo wanastahili kupewa heshima na hifadhi ya jamii badala ya kutelekezwa.
“Kila mmoja anapotimiza miaka 60 anastahili kulipwa pension na serikali, na tunasema kila mtu anastahili pension kwa sababu… huyu mzee aliyetengeneza taifa hili kwa kulima, kwa kujenga nyumba na kuzalisha, anajenga uchumi wa nchi hii…Kwanini wazee wa Zanzibar wapewe pension alafu nyinyi hampewi hata 100? Huu ni ubaguzi wa wazi kama nchi. Ahadi ya chama chetu kwenu ni kwamba wazee mnastahili heshima ya kupata matibabu first class bure na kupata pension”, ameeleza Heche.

Aidha, Heche ameeleza kuwa mfumo wa CHADEMA utazijengea uwezo jumuiya za wazee kupitia mikopo ya kibenki, zana za uzalishaji, na masoko ya uhakika akitolea mfano wa mfumo wa Kibbutz unaotumiwa nchini Israel na mifumo ya kijamii nchini Ujerumani. Amebainisha kuwa hatua hiyo itawafanya wazee waishi uzee wenye heshima na kujitegemea badala ya kuonekana mzigo kwa familia zao.
Akiunganisha ustawi wa wazee na sekta ya kilimo, Heche amesisitiza kuwa nchi yenye akili inapaswa kuchukulia kilimo kama suala la usalama wa taifa na kuwalipa wakulima ruzuku. Alikosoa utawala wa CCM kwa namna unavyoisimamia sekta ya kilimo nchini kwa kuendelea kutumia fedha nyingi kwa kuagiza bidhaa kama ngano kutoka nje ya nchi kama Urusi, Ukraine, na Saudi Arabia akisema bidhaa hizo zinaweza kuzalishwa katika ubora nchini Tanzania.

Pia, ameonya kuhusu hatari ya afya inayowakabili Watanzania kutokana na matumizi ya mbegu zilizobadilishwa vinasaba (GMO) na mafunzo duni ya vyakula vinavyoingizwa kutoka nje, akidai kuwa vinasababisha vijana wa miaka 40 hadi 50 kupatwa na kiharusi, shinikizo la damu, na tezi dume.
Heche amesisitiza kuwa CHADEMA ndicho chama pekee nchini kilichoandaa sera mbalimbali mahususi ikiwemo sera ya wazee, sera ya wanawake, na sera ya vijana ili kuinua kiwango cha umri wa kuishi nchini kufikia viwango vya nchi zilizoendelea.