Serikali ya Tanzania imebainisha kuwa inalenga kuimarisha zaidi uhusiano wake wa kiuchumi na nchi ya Italia kwa kuupanua kutoka biashara ya kawaida na kuelekeza nguvu katika uwekezaji wa teknolojia, maarifa, ubunifu pamoja na mageuzi ya kidijiti.
Msimamo huo umeelezwa tarehe 1 Oktoba 2026 mjini Cesena, Italia, wakati ujumbe wa Tanzania uliposhiriki katika jukwaa la EU-Tanzania Investment and Business Forum Roadshow, ikiwa ni sehemu ya ziara ya uhamasishaji uwekezaji barani Ulaya.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya amebainisha kuwa Tanzania inatafuta ushirikiano utakaobadili mwelekeo wa kiuchumi kupitia teknolojia na ubunifu.

Dkt. Chaya ameongeza kuwa Serikali inalenga uwekezaji utakaotoa matokeo yanayoshikika katika uchumi kupitia uzalishaji, uongezaji thamani, mauzo ya bidhaa nje ya nchi, ajira, uhamishaji wa teknolojia na maendeleo ya ujuzi.
Katika sekta ya uchumi wa kidijiti na teknolojia, kampuni na wawekezaji kutoka Italia wamealikwa kuwekeza katika maeneo ya kimkakati ikiwemo miundombinu ya kidijiti, usambazaji wa intaneti, vituo vya kuhifadhia data, teknolojia ya fedha (fintech), mfumo wa serikali mtandao, akili unde, pamoja na ukuzaji wa ujuzi wa kidijiti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, aliwasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji na kueleza utayari wa TISEZA katika kuwaunganisha wawekezaji wa Italia na fursa zilizopo.

Mbali na teknolojia na mageuzi ya kidijiti, majadiliano hayo pia yaliangazia uwekezaji katika sekta ya kilimo na usindikaji, nishati safi na jadidifu, pamoja na usafirishaji na lojistiki.
Ziara hiyo ya nchini Italia ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Jukwaa la Uwekezaji na Biashara la Tanzania na Umoja wa Ulaya (Tanzania–EU Investment and Business Forum 2027) linalotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam.
