Latest Posts

“SIO UHAINI, NI VITA YA KISIASA”, LISSU AANZA KUJITETEA KIZIMBANI, AANIKA SHAMBULIO LA RISASI, NA MAPAMBANO YA KISIASA YA MIAKA 20

Baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kukataa maombi yake ya kuachiwa huru na kumkuta na kesi ya kujibu, kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Antiphas Lissu, ilirejea tena mahakamani mchana wa leo Agosti 21, 2026 kwa ajili ya kuanza rasmi kwa utetezi wake

Kesi hiyo iliendelea mchana wa leo saa 9:48 mchana baada ya mapumziko mafupi yaliyotolewa na mahakama. Mara baada ya jopo la majaji kuingia ukumbuni, upande wa mashtaka ulitangaza kuwa upo tayari kuendelea kusikiliza utetezi wa mshitakiwa, na Lissu pia alithibitisha utayari wake

Hata hivyo, kabla ya kuanza utetezi wake, Lissu aliomba maelekezo ya mahakama kuhusu utaratibu wa mashahidi wake ambao tayari walikuwa wameruhusiwa kutoa ushahidi, akitaka kujua kama wanapaswa kuwepo ukumbini au watoke nje kwanza. Majaji walitoa maelekezo kuwa mashahidi wengine hawapaswi kuwepo ndani ya ukumbi wakati shahidi mwingine akiwa kizimbani

Kufuatia amri hiyo, viongozi waandamizi wa CHADEMA ambao walipangwa kuwa mashahidi wakiwemo John Mnyika, Amani Golugwa, na John Heche waliondoka ukumbuni ili kusubiri kuitwa kutoa ushahidi wao

Baada ya hapo, Lissu alisimama kama shahidi wa kwanza na kula kiapo kizimbani. Akianza kutoa ushahidi wake, Lissu alieleza kuwa sehemu ya kwanza ya utetezi wake inahusu maisha yake binafsi ili kuisaidia mahakama kuelewa yeye ni mtu wa namna gani. Alijitambulisha kama kiongozi wa chama cha kisiasa kilichosajiliwa kisheria, akishikilia nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa tangu tarehe 22 Januari 2025, nafasi ambayo alidumu nayo kwa takriban wiki tano au sita tu kabla ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini

Lissu alieleza kwa kina historia ya uongozi wake ndani ya CHADEMA, akibainisha kuwa alishikilia nafasi ya Umakamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara kwa miaka mitano tangu Desemba 2019 hadi Januari 22, 2025. Alikuwa Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama kuanzia mwaka 2010 hadi Septemba 7, 2017.

Kabla ya hapo, alihudumu kama Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa CHADEMA kuanzia takriban Julai 2004 hadi Novemba 2011, jambo ambalo lilimfanya adumu katika nafasi za juu kabisa za uongozi wa chama hicho kwa takriban miaka 20

Lissu aliendelea na ushahidi wake kwa kueleza kuwa nje ya CHADEMA, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Singida Mashariki (sasa inaitwa Ikungi Mashariki) kwa tiketi ya CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kuchaguliwa tena Oktoba 2015. Hata hivyo, hakumaliza kipindi chake cha ubunge kutokana na matukio ya kutisha yaliyompata mnamo Septemba 7, 2017

Siku hiyo, akiwa Dodoma akihudhuria vikao vya Bunge, alifuatwa kutoka bungeni hadi kwenye makazi yake rasmi ambapo alishambuliwa kwa risasi nyingi sana na watu ambao serikali inawaita “watu wasiojulikana”.  Kufuatia shambulio hilo, alikimbizwa Hospitali ya Dodoma na kisha kupelekwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambapo alitibiwa kwa miezi minne hadi Januari 6, 2018. Baadaye, alihamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambapo alikuwa akitibiwa hadi Januari 2022, huku akifanyiwa jumla ya upasuaji (operations) 25 kati ya Nairobi na Ubelgiji

Lissu aliweka wazi kuwa mnamo Juni 29, 2019, aliyekuwa Spika wa Bunge, marehemu Job Ndugai, alimvua ubunge kwa madai kuwa alikuwa “mtoro” bungeni kwa takriban miaka miwili. Alilalamika kuwa bunge na serikali vilikataa katakata kumlipia hata senti moja ya gharama za matibabu yake, licha ya uwepo wa sharia inayoelekeza kuwa mbunge anayeumia akiwa kazini anapaswa kutibiwa kwa gharama za bunge.

Alikumbusha kuwa akiwa bungeni, alikuwa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani (kiongozi namba mbili akimsaidia Freeman Mbowe), pamoja na msemaji mkuu wa masuala ya katiba, sheria, muungano, na mwanasheria mkuu kivuli

Katika hoja yake, Lissu aliweka wazi kuwa haoni kama amefanya kosa lolote la uhaini na kusema, “Kilichonileta hapa kwenye hii kesi leo si uhaini bali ni mgogoro mkubwa wa kisiasa, mfumo huru wa uchaguzi na katiba; kilicholeta hapa ni vita ya kisiasa”.

Aliongeza kuwa aliongoza harakati za kupigania Katiba Mpya na mfumo huru wa uchaguzi bungeni kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 kama Mjumbe wa Bunge Maalumu la KatibaPia, alitaja kuwa alichaguliwa na mawakili kuwa Rais wa Tanganyika Law Society (TLS) mnamo Machi/Aprili 2017 hadi aliposhambuliwa mnamo Septemba 17, 2017, akisisitiza kuwa “huwezi kuwa Rais wa TLS kama wewe ni mtu lainilaini”

Kimataifa, alijitambulisha kama Makamu Mwenyekiti wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (International Democrat Union – IDU) anayewakilisha bara zima la Afrika, shirika linalounganisha vyama vya kidemokrasia kutoka nchi zaidi ya 80 duniani, akidai kuwa yeye ni mtu wa heshima kubwa ndani na nje ya nchi kwa sababu ya msimamo wake wa kupigania haki

Lissu aliorodhesha tuzo mbalimbali za kimataifa alizowahi kutunukiwa kutokana na msimamo wake wa kupigania haki na demokrasia. Mnamo Mei 2011, alipewa tuzo ya heshima ya kuwa Mwenza wa Kimataifa (International Fellow) wa Chuo Kikuu cha Bridgeport kilichopo Connecticut, Marekani. Katika maelezo ya tuzo hiyo, walisema walimzawadia kwa ajili ya kupigania haki za binadamu, mazingira, na demokrasia nchini Tanzania na Bara la Afrika

Mnamo Desemba 2020, alitunukiwa heshima nyingine na IDU, tuzo inayoitwa “Bush-Thatcher Award for Freedom” kwa ajili ya kupigania haki bora, utawala bora, na demokrasia Afrika.

Mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa hata baada ya kufunguliwa mashtaka haya na kukaa gerezani, heshima yake kitaifa na kimataifa haijapungua bali imeongezeka. Alifichua kuwa taasisi za kitaifa, kikanda, na kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Ulaya (EU), na Jumuiya ya Madola zimetangaza kuwa mashtaka yake ni ya kisiasa na kutaka aachiwe huru bila masharti.

Baraza la Haki za Binadamu la UN limetaka pia alipwe fidia, huku nchi za Jumuiya ya Ulaya na Marekani zikisitisha baadhi ya misaada kwa Tanzania kwa sababu ya kesi hiyo. Aliongeza kuwa kwa sasa Bunge la Marekani linajadili muswada wa sheria wa kuziwekea vikwazo Serikali ya Tanzania na viongozi wake kutokana na mashtaka yake, akisema dunia haiwezi kumpigania mtu ambaye ni mhalifu au “wa hovyo”

Lissu alifafanua kuwa shtaka linalomkabili linatokana na kauli aliyoitoa tarehe 3 Aprili 2025 kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana (2025). Alitaka mahakama irekodi kuwa ana uzoefu mkubwa sana wa masuala ya uchaguzi nchini, kwani amepiga kura tangu mwaka 1985 na kushiriki katika uchaguzi mkuu wowote ama kama mpiga kura au kama mgombea, isipokuwa ule wa mwaka 2000 (alikuwa masomoni Marekani) na mwaka 2025 (alikuwa gerezani)

Katika Uchaguzi wa mwaka 1995, alisema alisimamisha masomo yake ya ngazi ya uzamili (Masters) ili kurudi Tanzania kugombea Ubunge Jimbo la Singida Kusini

Pia, ameshiriki kama wakili mkuu wa kesi za uchaguzi za CHADEMA tangu mwaka 2005 na kufanya utafiti mkubwa tangu mwaka 2021 hadi alipokamatwa kuhusu “mfumo wa uchaguzi wa Tanzania na “uchafu wake” tangu enzi za ukoloni”

Alihitimisha kuwa hakuna hoja yoyote ya uchaguzi ya CHADEMA kwa miaka 10 iliyopita ambayo haijapita mikononi mwake, na ndiyo maana amekuwa mstari wa mbele kupigania mfumo huru wa uchaguzi

Baada ya Lissu kumaliza kutoa maelezo hayo yaliyochukua takriban saa mbili na nusu hadi kufikia saa 11:00 jioni, jopo la majaji liliahirisha kesi hiyo kutokana na muda wa mahakama kuisha. Kesi imeahirishwa hadi Jumatatu, Agosti 24, 2026, ambapo Tundu Lissu atatarajiwa kuendelea kutoa sehemu inayofuata ya ushahidi wake wa utetezi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!