Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametoa wito kwa jamii kurejea katika misingi imara ya malezi ya vijana inayozingatia kumjua Mungu, kufanya kazi kwa bidii, na kupenda masomo ili kujenga taifa lenye uadilifu na ujuzi
Akizungumza katika Ibada ya Misa Takatifu Maalum ya Wanajumuiya wa Uru Seminari iliyofanyika jana katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kristo Mchungaji Mwema, Tabata Kimanga mkoani Dar es Salaam, Dkt. Nchimbi amekumbusha wajibu wa kila mbatizwa kuwa ‘mmishionari’ anayeleta mabadiliko chanya katika jamii.

Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa waumini wanapaswa kutumia nafasi zao mahali walipo ili kuleta tofauti kwa kutenda haki na kueneza upendo.
“Tukumbuke wito wetu muhimu wa kwenda kutakatifuza malimwengu mahali ulipo pawe na tofauti… uwepo wako mahali pale ulete matumaini kwa watu, ulete upendo, ulete haki, ulete matumaini ambayo yanamfanya mtu aone leo ni bora kuliko jana,” amesema Makamu wa Rais
Aidha, amewataka vijana kuweka juhudi katika masomo na kuepuka kutamani mafanikio ya haraka bila kufanya kazi. “Kusoma kunaleta ujuzi, kutosoma kunazalisha tabia ya kupenda njia za mkato,” ameonya Makamu wa Rais
Katika hatua nyingine, Dkt. Nchimbi amewahakikishia waumini kuwa serikali inathamini na itaendelea kudhamini mchango wa taasisi za dini katika kutoa huduma za kijamii. Amesema kuwa taasisi hizo zimekuwa washirika wakubwa wa serikali, hususan katika sekta za elimu na afya nchini kote
Makamu wa Rais amehitimisha kwa kutoa wito kwa Watanzania kuendeleza umoja, kufanya kazi kwa juhudi, na kuendelea kuiombea nchi ili iendelee kuwa na amani na ustawi
