Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, ameeleza masikitiko yake makubwa kufuatia kile alichokiita kuwa ni mkakati ulioratibiwa na serikali kuudhoofisha uongozi wa sasa wa chama hicho, akitolea mfano kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wao, Tundu Lissu
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 21, 2026, katika Ofisi za CHADEMA Makao Makuu mara baada ya kutoka mahakamani kufuatilia kesi hiyo, Heche amebainisha kuwa chama hicho kinapitia kipindi kigumu ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka thelathini iliyopita
“Na leo mimi nimesikitishwa sana na kilichotokea na ni muhimu mkaelewa tangu tuchaguliwe mpaka sasa leo ni siku ya chama hiki kimekuwepo tangu mwaka 92 hakijawahi kupita misukosuko mikubwa kama hii ambayo tunapitia leo,” amesema Heche kwa masikitiko
Heche ameanika takwimu zinazoonyesha jinsi chama hicho kinavyowekewa vizuizi vya kiutendaji, akifafanua kuwa kati ya siku 576 tangu uongozi wao uingie madarakani, chama hicho kimezuiliwa kufanya kazi zake za kisiasa kwa siku 309. Ameongeza kuwa hali hiyo imewaacha na siku 267 tu za kufanya kazi kikamilifu, ambazo hazijatimiza hata mwaka mmoja wa utendaji, lakini bado watawala wamekuwa wakihangaika kukizuia chama hicho
Aidha, Heche ameeleza kuwa katika kipindi chote hicho cha siku 576, mwenyekiti wao ameweza kukaa ofisini kwa siku chache tu kutokana na vikwazo na changamoto mbalimbali za kisheria na kiusalama

Amehusisha matukio hayo ya sasa na historia ya Tundu Lissu ya kushambuliwa pindi anapopata nafasi za uongozi.
“Eleweni kwamba historia ya huyu mtu ni ya aina gani na wanamuogopa kwa kiasi gani. Huyu mwenyekiti alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa TLS alikaa madarakani siku ngapi? Alikaa chini ya miezi sita akapigwa risasi,” amesisitiza Heche, akionesha kuwa mashtaka na misukosuko ya sasa ni muendelezo wa hofu ileile dhidi ya mwenyekiti wao