Watu watano wamefariki dunia na wengine wanane kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Coaster yenye namba za usajili T.151 DMC kuacha njia na kutumbukia bondeni katika eneo la Vuga, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
Ajali hiyo imetokea leo, Agosti 18, 2026, majira ya saa 7:30 mchana, katika barabara ya Mombo–Lushoto.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, gari hilo lilikuwa likitokea Tanga Mjini kuelekea Ngwashi na lilikuwa likiendeshwa na Ally Dione.
Katika ajali hiyo, watu watano wamepoteza maisha, ambao hadi sasa hawajatambuliwa majina. Marehemu hao ni wanaume wawili wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 hadi 45, wanawake wawili wenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 25 hadi 35, pamoja na mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi sita.
Watu wengine wanane wamejeruhiwa na wamelazwa katika Kituo cha Afya Soni, Wilaya ya Lushoto, ambapo wanaendelea kupatiwa matibabu.
Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa ajali hiyo imetokana na uzembe wa dereva, ambaye alishindwa kulimudu gari na kusababisha liache barabara na kutumbukia bondeni.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa ajili ya uchunguzi, utambuzi na taratibu nyingine za kisheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linaendelea na uchunguzi ili kubaini kwa kina chanzo na mazingira ya ajali hiyo.
Jeshi hilo limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuwa makini wanapokuwa barabarani na kuhakikisha wanaendesha kwa umakini ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Aidha, wananchi na watumiaji wengine wa barabara wamekumbushwa kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja.