Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema juhudi za kusambaza teknolojia za nishati safi ya kupikia nchini lazima ziende sambamba na mabadiliko ya mila, desturi, na mitazamo inayorudisha nyuma mikakati ya Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anatumia nishati salama na safi ya kupikia.
Ndejembi ameyasema hayo mnamo Agosti 11, 2026, huko Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, wakati wa Mdahalo wa Nishati Safi ulioandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) na kukutanisha wadau wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha, na asasi za kiraia.

Akifafanua msingi wa mabadiliko hayo, Waziri Ndejembi amesema, “licha ya kuwa na mkakati wa nishati safi ya kupikia, tusipowekeza katika kubadili mila na desturi zetu tutajikuta palepale. Wakati tunasukuma matumizi ya teknolojia, tuwekeze pia katika kubadili mitazamo ya Watanzania kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia”.
Waziri Ndejembi amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka sera na uwekezaji uliowezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupanda kutoka asilimia 6.9 (mwaka 2021) hadi kufikia asilimia 28.6 (mwaka 2025). Amesema hatua hizo zimefanikiwa kupitia ruzuku za mitungi ya gesi, miradi ya kulipia majiko ya umeme kupitia bili (on-bill financing), na kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye gesi, mitungi, na mita janja.

Hata hivyo, amebainisha ukubwa wa kazi iliyopo kwenye taasisi kubwa zinazolisha zaidi ya watu 100 kwa siku. Ameeleza kuwa kwa sasa ni taasisi 2,616 pekee kati ya taasisi 31,395 zinazotumia nishati safi ya kupikia hali inayoonesha ukubwa wa kazi iliyopo mbele katika kufikia malengo yaliyowekwa.
Kutokana na ukubwa wa mahitaji hayo, Ndejembi amesema mabadiliko hayawezi kufanikishwa kwa kutegemea bajeti ya Serikali pekee, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na uhamasishaji wa rasilimali fedha.

Ametoa wito kwa taasisi za fedha kubuni mikopo nafuu itakayowezesha shule, hospitali na taasisi nyingine kuwekeza katika nishati safi bila kulazimika kulipa gharama zote za awali kwa wakati mmoja.
Pia ameihimiza sekta binafsi kuja na mifumo bunifu ya kifedha, ikiwemo malipo kwa awamu na mikopo yenye masharti nafuu.