Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanzo Mpya Foundation, Mussa Ryoba, ameendelea kugusa maisha ya wananchi kwa kutoa msaada wa Televisheni aina ya Smart TV yenye ukubwa wa inchi 55 kwa wajumbe wa kijiwe maarufu cha Juma Kahawa, kilichopo mjini Tarime.
Msaada huo umetolewa kufuatia maombi yaliyowasilishwa na wajumbe wa kijiwe hicho, wakihitaji televisheni itakayowawezesha kupata habari mbalimbali pamoja na burudani.
Katika hafla ya kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alikuwa mgeni rasmi, akiongozana na Mwenyekiti wa Mwanzo Mpya Foundation Wilaya ya Tarime, Bw. Mashaka Butiku,
Viongozi hao walipokelewa na wajumbe wa kijiwe hicho wakiongozwa na msemaji wao Bw. Daniel Komote pamoja na wadau wa kijiwe hicho.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wajumbe wa kijiwe hicho walimshukuru Mkurugenzi wa Mwanzo Mpya Foundation, Mussa Ryoba, kwa msaada huo, wakisema televisheni hiyo itawasaidia kufuatilia habari za ndani na nje ya nchi, kujifunza mambo mbalimbali pamoja na kupata burudani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alitumia fursa hiyo kusikiliza na kupokea kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi pamoja na wadau wa kijiwe hicho, huku akitoa maelekezo kwa mamlaka husika kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi.
Hatua hiyo ya Mwanzo Mpya Foundation inaendelea kuonyesha dhamira ya taasisi hiyo ya kushirikiana na jamii katika kuleta maendeleo, kuimarisha upatikanaji wa taarifa na kuchochea mshikamano miongoni mwa wananchi.
Aidha DC Gowele ametumia wasaa huo kusikiliza na kutatua kero za Wananchi na wadau hao.
