Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Fabian Ngajilo, ameiomba Serikali kupitia Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kuharakisha ujenzi wa Barabara ya Mchepuo ya Iringa (Iringa Bypass), akisema kukamilika kwake kutasaidia kupunguza msongamano wa magari ndani ya Manispaa ya Iringa.
Ngajilo ametoa ombi hilo katika mkutano wake na wananchi uliolenga kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili, ambapo suala la ujenzi wa barabara hiyo lilitajwa kuwa miongoni mwa mahitaji muhimu ya wakazi wa maeneo yanayopitiwa na mradi.

Barabara hiyo inayounganisha eneo la Igumbilo na upande wa Kihesa-Kilolo kuelekea barabara ya Dodoma–Iringa, ina urefu wa takribani kilomita 7.3 na inajengwa kwa kiwango cha lami, ikigharimu Sh bilioni 41.6 na unatekelezwa na SINOHYDRO Corporation Limited chini ya usimamizi wa TANROADS.
Kwa mujibu wa TANROADS, mradi huo umebuniwa pamoja na maboresho mengine yatakayowezesha magari kupita kwa ufanisi zaidi, ikiwemo maeneo ya kupandia, taa za barabarani na maegesho ya malori, huku lengo likiwa ni kupunguza msongamano na kuwezesha barabara hiyo kuhudumia magari yenye uzito mkubwa.

Hata hivyo, kwa sasa ujenzi wa barabara hiyo umesimama, hali iliyomsukuma Mbunge Ngajilo kuomba Serikali kuharakisha utekelezaji wake ili wananchi waanze kunufaika na umuhimu wa mradi huo, hususan katika kupunguza msongamano wa magari yanayoingia na kutoka katika maeneo ya mjini.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kihesa Hosea Kabelege ameomba, mara ujenzi utakapoendelea wanaoishi katika maeneo jirani wapewe kipaumbele katika ajira za muda zitakazotokana na mradi huo.

Amesema hatua hiyo itasaidia wananchi kunufaika kiuchumi wakati wakisubiri manufaa makubwa yatakayopatikana baada ya barabara hiyo kukamilika, akieleza kuwa wakazi wa maeneo hayo pia watakuwa sehemu ya kwanza kulinda na kutunza miundombinu itakayojengwa.
Mradi wa Iringa Bypass umeelezwa na Serikali kuwa ni miongoni mwa miradi muhimu ya kimkakati kwa Manispaa ya Iringa, kutokana na mchango wake unaotarajiwa katika kupunguza msongamano wa magari, kuboresha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika mji huo.
