Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, amewapa wiki mbili Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani humo kuandaa mikakati mipya ya kukuza sekta ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kuongeza tija katika uzalishaji na kuinua kipato pamoja na uchumi wa wananchi.
Malima ametoa agizo hilo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Moka, Wilaya ya Lindi, ambapo amesisitiza umuhimu wa Halmashauri kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika sekta ya kilimo ili kuchochea maendeleo ya wananchi.

Amesema kilimo ni miongoni mwa sekta muhimu katika kuinua maisha ya wananchi, hivyo ni wajibu wa Halmashauri kuhakikisha zinaweka mikakati inayolenga kuongeza uzalishaji, kuwawezesha wakulima na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao.
Malima amewataka Wakurugenzi kuwasilisha mikakati hiyo ndani ya wiki mbili, huku akisisitiza kuwa mipango hiyo inapaswa kuwa na matokeo yanayoonekana katika kuongeza tija ya kilimo na kuboresha maisha ya wananchi wa Mkoa wa Lindi.
