Changamoto ya utoro kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Matengo iliyopo Halmashauri ya Mbinga Mji mkoani Ruvuma imemalizika baada ya serikali kuleta mradi wa darasa janja katika shule hiyo, jambo ambalo limewafanya wanafunzi kupenda kusoma na kuacha tabia ya utoro shuleni.
Akimuelezea Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, utekelezaji wa mradi wa madarasa mawili ambayo ni darasa janja pamoja na darasa la TEHAMA yaliyopo katika Shule ya Msingi Matengo, iliyopo Halmashauri ya Mbinga Mji mkoani Ruvuma, tarehe 14/9/2026, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Matengo, Hawa Nambwaja, amesema ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 331, ikiwemo vyumba tisa vya madarasa, jengo la utawala na vyoo vya kisasa. Aidha, vifaa vya TEHAMA na ujuzi wa kidijitali vimegharimu kiasi cha shilingi milioni 39.

Amesema darasa janja lina kifaa cha kurekodi namna mwalimu anavyofundisha wanafunzi, jambo linalomsaidia Mwalimu Mkuu kuona na kufuatilia mwenendo wa ufundishaji wa walimu wake.
Kelvin Mapunda ni Diwani wa Kata ya Matarawe iliyopo Halmashauri ya Mbinga Mji. Amesema darasa janja limesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa utoro wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Matengo.
Baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo katika Shule ya Msingi Matengo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, amesema serikali inaendelea kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika jamii, ikiwemo uboreshaji wa sekta ya elimu, ambapo amepongeza uwepo wa elimu ya kisasa katika shule hiyo ya msingi.
